Akili ‘napo pumbaa, haina iogopacho
Huwa yajisabilia, kwa chochote kitukacho
Hwona kifo chachelewa, mana ‘ndo tu ingojacho
Akili ‘shayo pumbaa, haiogopi vitisho
Haichi myoto ya nari, wala adhabu nzito
Haimchi jemedari, na mizingaye mizito
Itishwe kwa masumari, yaliyokolezwa moto
Kwayo ishavyo pumbaa, faru yamuona popo
‘Napo pumbaa Akili, haina vya kusemezwa
‘Sipoteze zako mali,’kadhani ‘taigeuza
Iaminicho ndo kweli, ndio hicho ‘takifanza
‘Yache Akili pumbavu, ifate upumbavuwe
Hamad Hamad
27 Aprili 2014
Dodoma