Kila lugha ina kanuni zake zinazoiongoza na kwa hakika ndio misingi ambayo kwayo lugha hiyo husimamia. Katika ujumla wake, kanuni hizo huitwa sarufi, lakini katika uchambuzi wake, taaluma ya sayansi za lugha, isimu, hukichambua kila kiwango na kipenu cha sarufi kwa mawanda na vina vyake. Ndiyo maana ilimu ikaitwa ilimu, kwa kuwa huzama na kujichawanya.
Hata hivyo, lugha zinazokutikana kwenye kundi moja, kama vile Kiswahili kinavyoambiwa kuwa kimo kwenye kundi la lugha za Kibantu, hujikuta pia na mfanano kwenye sehemu kubwa (au pengine yote) ya sarufi yake. Kwa mfano, namna maneno yanavyoundika kwenye umoja na wingi, mjengeko wa maneno katika kuunda sentensi, na kadhalika. Lugha zinazotafautiana makundi, kama vile Kiingereza na Kiswahili, hutafautiana pia kimsingi kwenye kanuni zake.
Leo tuzungumzie kidogo kwenye kanuni ya upatanishi wa kisarufi, ambayo inasema muundo wa maneno kwenye sentensi hutegemea kiima (sehemu inayokaliwa au inayowakilisha mtenda kwenye sentensi). Umoja, wingi, kundi la maneno (ngeli wanavyoiita wengine), au hata aina za maneno huwa zinalingana na hicho kiima.
Kwa mfano, katika sentensi “kuku wangu analalia mibani”, kivumishi cha kumiliki ‘wangu’ na kipashio cha awali ‘a-‘ kwenye kitenzi ‘analalia’ ni kwa sababu nomino ‘Kuku’ iko kwenye kundi la maneno la ‘YU-A-WA’. Kama hapo penye mahala pa kuku ingelikuwepo nomino kutoka kundi jengine, kama vile KI-VI au LI-YA, basi kungelikuwa na mabadiliko. Mathalani tungeweka ‘kisu’ au ‘tunda’, sentensi ingesomeka: ‘kisu changu kinalalia mibani’ au ‘tunda langu linalalia mibani’ (hii mifano ya kisu na tunda huenda si sahihi kimaana lakini ni sahihi kwenye mjengeko wa maneno na sentensi).
Hoja ninayojaribu kujenga hapa ni kwamba upatanisho wa kisarufi kwenye Kiswahili upo na una kanuni yake. Kanuni hiyo ni kwamba Kiima ndicho hutawala katika sentensi na kama ni kwenye kifungu cha maneno kisichokuwa sentensi kamili, basi nomino ndiyo hutawala. Ndipo hapo linapokuja hilo swali lililobeba jina la makala hii. Je, upatanisho wa kisarufi kwenye Kiswahili unaongoza iwe ‘kiasi cha’ au ‘kiasi ya’?
Maelezo ya hapo juu tayari yana jawabu. Kwamba kwa kuwa ‘kiasi’ hapo ndiyo nomino na kwa kuwa nomino ndiyo inayoongoza uambishaji kwenye maneno mengine yanayohusiana nayo kwenye sentensi, basi kundi lake ndilo la kuakisika kwenye kipashio cha ‘-a unganifu’ kinachofuatia hapo. Kiasi imo kwenye kundi la KI-VI na sio I-ZI au U-I. Hivyo tungepaswa kusema ‘kiasi cha’ na sio ‘kiasi ya’. Hiyo itakuja hata kama kilichoko mbele ya ‘-a unganifu’ ni neno kutoka ngeli ya YU-A-WA, yaani kama mtu au watu, au mnyama, ndege, na kadhalika.
Kwa hivyo, haitakuwa sahihi kusema “kiasi ya watu kumi wamekufa” bali sahihi ni kusema “kiasi cha watu kumi wamekufa”.