KISWAHILI KINA WENYEWE

Idhaa za kimataifa na Kiswahili Sanifu

Makala hii inajaribu kuuliza swali hili: Je, mitandao ya idhaa za Kiswahili za redio za kimataifa zina wajibu kwenye ujengaji wa Kiswahili Sanifu. Si makala yenye majibu, bali inayotaka tu kulifafanua swali lenyewe ili watafiti waje na majibu.

Lakini kabla ya kuingia undani wa swali lenyewe, kuna mambo yanayohitaji kufafanuliwa. La kwanza ni maana na matumizi ya neno “mtandao“ kama linavyotumika hapa, ambalo linakusudiwa mitandao ya intaneti, ambayo wengine huita wavuti au tovuti.

Ukweli ni kwamba licha ya kuwa maeneo ambayo Kiswahili kinazungumzwa kama lugha ya kwanza, ya pili, au ya tatu yana umasikini wa kipato, matumizi ya njia hii mpya ya mawasiliano yanakuja juu kwa kasi na, kidogo kidogo, yameanza kuchukuwa nafasi ya njia za kawaida za mawasiliano na taaluma kama vile magazeti na vitabu.

Katika hili, hoja ni kwamba madhali mitandao hiyo inazidi kupata ufuasi kadiri siku zinavyosonga mbele, basi nacho Kiswahili kinachotumiwa humo kina nafasi kubwa ya kuathiri uelewa wa watu kuhusu lugha hiyo na hata matumizi yake. Ikiwa, kwa mfano, wanaona maneno “takwa” na “kiasi cha” yanatumika mara kwa mara kwenye vyombo hivyo, basi hatimaye watadhani kwamba hayo ni maneno sahihi kwenye Kiswahili na yakaingia kwenye Kiswahili kilichosanifiwa.

Dhana ya Kiswahili Sanifu

La pili kulifafanua ni dhana ya “Kiswahili Sanifu“, maana kama jina lenyewe linavyojieleza hicho ni Kiswahili kilichosanifiwa. Kusanifu ni kutengeneza au kusawiri. Je, matumizi ya Kiswahili kwenye mitandao ya idhaa hiyo inaweza “kutengeneza” maneno yanayoingia kwenye Kiswahili na hivyo kuwa na dhima katika “usanifishaji” huo?

Kuna hoja kwamba usanifishaji wa lugha si jambo linalofanyika na kumalizika, bali ni utaratibu unaoanza na kuendelea kadiri lugha hiyo inavyokuwepo kwenye matumizi – wenye Kiswahili chao siku hizi huita utaratibu huo kwa jina la “mchakato” (tafadhali usihusishe na msamiati mpya wa “kuchakachua” uliongia kwenye siasa za uchaguzi nchini Tanzania hivi sasa). Kwa hivyo, pale mwaka 1922, chombo kilichoundwa na serikali ya kikoloni na kupewa jina la Baraza la Kiswahili la Afrika ya Mashariki, kilipokiteua Kiunguja Mjini kuwa lahaja inayowakilisha Kiswahili Sanifu, ulikuwa ni mwanzo tu, na wala si mwisho wa usanifishaji.

Mimi si miongoni mwa watu wanaokubali kwamba Kiswahili kizuri ni hicho cha Unguja Mjini, ingawa ni sehemu ya lahaja zangu binafsi. Ila hiyo ni mada ya wakati mwengine. Kwa sasa, na kwa ufupi, tukubaliane kuwa wakati huo, ilikubalika kwamba lahaja ya Kiunguja Mjini ndiyo isanifishwe (yaani itengenezwe, irembwerembwe, isarifiwe) na kuwa Kiswahili Sanifu. Kwa kuwa uamuzi huo haujabatilishwa hadi sasa, basi unabakia kuwa kama ulivyo, yaani msingi wa Kiswahili Sanifu ni kile kinachozungumzwa Unguja Mjini.

Je, kwa kiasi gani mitandao ya idhaa za Kiswahili za kimataifa zinazingatia kujengwa na au kubomolewa kwa Kiswahili hicho linapokuja suala la usanifu wa lugha ya Kiswahili?

Idhaa za Kiswahili za Kimataifa

Jambo la tatu ni sababu ya kuzichagua Idhaa za Kiswahili za Kiswahili za Kimataifa kama vile Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Sauti ya Marekani (VoA) na Sauti ya Ujerumani (DW). Sababu kubwa na ya msingi ni kiwango cha hadhira ambacho Idhaa hizo zinacho ndani na nje ya Afrika ya Mashariki na Kati na hata nje ya hapo, kwani uzoefu unaonesha kuwa matumizi ya mitandao ni makubwa zaidi nje ya eneo hilo, kuliko ndani yake, na ambako Kiswahili hakizungumzwi si kama lugha ya kwanza, ya pili wala ya tatu.

Idhaa hizo zimeanza kuchapisha makala na taarifa zake mitandaoni takribani miaka 20 tu iliyopita, lakini takribani miaka 30 kabla ya hapo zilikuwa zikitangaza kupitia redio tu na kujizolea hadhira kubwa katika maeneo hayo. Kutokana na mageuzi hayo makubwa kwenye teknolojia ya mawasiliano, hivi sasa watu kwenye maeneo hayo wanaweza kuzisoma makala na taarifa za habari moja kwa moja kupitia mitandao, kama vile ambavyo wangeliweza kusoma habari kutoka magazetini. Je, wanaposoma habari hizo na wakakutana na misamiati au miundo mipya ya maneno, ambayo haikuwahi kufahamika kwao, wanaikubali na kuipokea na wao kuanza kuitumia?

Kwa mfano, ni matumizi ya vifungu vya maneno “mwisho wa siku….” au “baada ya yote…” yaliyokopwa kama yalivyochukuliwa kutoka Kiingereza “at the end of the day…..” na “after all…”, ingawa kuna maneno ya Kiswahili kama vile “hatimaye” na “pamoja na hayo…”.

Ushahidi wa kihistoria

Ushahidi wa kawaida unaeleza kwamba idhaa hizo zimejizolea hadhira kubwa kwenye eneo hilo kutokana na sababu kadhaa; mojawapo ni uwezo wake wa kutangaza yale ambayo hayasemwi kwenye redio za maeneo hayo. Kiu ya habari tafauti, wasemavyo wengine.

Msingi wa hoja ni kwamba kwa kuwa vyombo hivyo vya habari vya kimataifa vimejijengea sifa ya kuaminiwa na hadhira yake kama vyombo vinavyotoa taarifa sahihi ya kimataifa, kikanda na kitaifa, basi njia inayotumiwa na vyombo hivyo – lugha kwa mintarafu ya makala haya – ina uwezekano mkubwa wa kuaminika na hadhira hiyo.

Na kwa kuwa moja ya athari za vyombo vya habari ni kuigwa kwa ujumbe wake, basi uwezekano wa lugha hiyo kuigwa ni mkubwa. Laiti ikiwa idhaa hizo zinakijenga Kiswahili Sanifu kwenye mitandao yake, basi athari yake ni kukijenga, bali ni kinyume chake ni sawa pia.

Ushahidi unaonesha kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao hiyo ya idhaa za Kiswahili inazidi kupanda kila uchao. Sehemu moja ya watumiaji hao ni wanafunzi ya Kiswahili nje ya eneo la Afrika ya Mashariki na Kati, kwa mintarafu ya Ulaya, Marekani na Asia, ambao wanatumia mitandao ya idhaa hizo kama sehemu ya mafunzo yao ya lugha ya Kiswahili.

Kwa hivyo, wakati hadhira hiyo ikiongezeka, ni muhimu kupima usahihi na usanifu wa matumizi ya lugha kwenye mitandao hiyo.

Kama nilivyotangulia kusema, sijaandika makala ya kufafanua dhima ya mitandao ya idhaa za Kiswahili za Kimataifa katika kukijenga Kiswahili Sanifu, bali nililofanya hasa ni kulifafanua swali nililouliza. Je, kuna mwenye majibu?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.