Haliwa katu haliwa, lau hatutaliwanya
Haliwa tena haliwa, tukiliachia mwanya
Haliwa mbona haliwa, tusijapojikushanya
Nga la kuwa haliwanywa, lisilowanywa haliwa
Haliwa hili haliwa, kiwa tutatulizana
Haliwa kamwe haliwa, miye nawambia tena
Baratu hili haliwa, ngojani mutajaona
Nga la kuwa haliwanywa, lisilowanywa haliwa
Haliwa jama haliwa, shoti tuwanye kikweli
Na tusipo halitawa, na tuwanye kikatili
Halitawa tukituwa, tupambane kulli hali
Nga la kuwa haliwanywa, lisipowanywa haliwa
Tukiliwanya litawa, kama tutawana kweli
Ila kwa hivi haliwa, madhli tuna zohali
Na kwa tushavyojigawa, kuwa hili ni muhali
E jamaa tuwanyeni nye!, lisipowanywa haliwa
Salma O. Hamad
Zanzibar
28 Februari 2014