Nimo ndani ya jahazi, nisi hata abiria
Jahazi lishehenezi, chelezoni laelea
Viwimbi vichezichezi, mbavuni vyajongelea
Nazikusanya pumzi, naanza kushahadia
Naanza kushahadia, mana sijui lendako
Kwa kuwa si abiria, kuulizia ni mwiko
Polepole lasogea, nami nazidi fukuto
Nawaona abiria, wana dalili za rapo
Abiria raparapa, washapandisha mapepo
Pepo hao kwa hakika, ni khofu ya waendako
Hawajui watafika, au watafia papo
Tamaa natamauka, walipo nami ni papo
Nyumbani watu wangoja, nilotumwa hayafise
Nende hawape faraja, ya shida na visa vyose
Washachoka ngojangoja, wataka leo nifike
Hawaeleze kwa hoja, mojamoja mambo yose
Utumwa niKiupata, taomba Rabi nifike
Sifa nyingi tazipata, kumbukumbuni niwekwe
Mama yangu atacheka, moyoni afurahike
Ela nisipoupata, na litote lisifike
Na litote lisifike, lizame nisonekane
Lizame nisitafutwe, lende chini lisakame
Lawama zisinipate, ziwaandame wengine
Tuliombee lifike, tuliombee kwa shime
Hamad Hamad
20 Februari 2014
Dodoma