Najisikia furaha, kuwa nawanwa ni wana
Nyumbani ninapongia, kelele ‘kapigishana
Wakaanza salimia, kwa salam ziso jina
Ila huwa naridhia, kuona miye nawanwa
Wana waniwaniapo, wakaanza pakatana
Wakakaa nikaapo, nyajihi kutazamana
Tukafanya vichekesho, vya baba na wake wana
Hapo ndipo nipendapo, kuwa nawanwa ni wana
Waniwania kwa hamu, kwa pamoja himahima
Hawataki panga zamu, wakawa wapokezana
Kwa misingi ya nidhamu, wawana tukawanana
Na mapenzi yakadumu, baba kuwanwa ni wana
Hamad Hamad
5 Septemba 2013
Zanzibar