Nilitoka ni mzima, nenda na safari zangu
Hadi njiani hakwama, kwa kudra zake mungu
Jimwiba lilinichoma, ukagwaya mwili wangu
Nerudishwa kwa vitanga, wenibeba walimwengu
Tumboni nafungwa kanga, nimudu pumzi zangu
Uso wangu umefinga, yamenijaa matungu
Watu wakakusanyika,wa tele nyumbani mwangu
Wakaanza hangaika, kunitibu donda langu
Wote wanahuzunika, nilikavyo mlimwengu
Wakakutana wavyele, wambali na majirani
Zikamiminika pole, lukuki wa milioni
Maumivu pale pale, utasema hayaoni
Donda limenichanganya, kutwa ninahangaika
Kila mara nalibinya, ati napunguza taka
Nalo bado lanyekenya, mimaji latiririka
Lipatiwe dawa gani donda lipate tibika!
Wa dua, wa qur-ani, wa makombe kuandika
Wa vidonge, wa majani, dawa zote metumika
Donda limekuwa sugu, sili, siogi, silali
Donda lafanya vurugu, lanitwika idhilali
Na vinzi na vinyigu, vyaidadisi ajali
Kiumizacho zaidi, donda lisitake pona
Vinzi vimeshitadi, kutwa kucha walin’gon’ga
Vinaniumiza hadi, ila sina la kufanya
Waganga na waganguzi, hawatambui kulala
Magwiji na wanagenzi, wanaiona thaqala
Yakapangwa maamuzi, ije tiba mbadala
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto!!
Wa mbadala kungia, donda wakalichunguza
Haraka wakachupia, chuma kwenda kuunguza
Tiba waliyoamua, vidudu kuangamiza
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto
“Tuviunguze vidudu, donda vinolitafuna
Mana vyaleta vurugu, na donda halitapona
Vikipata vuguvugu, uhai hivi havina”
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto
Donda lilivyoshamiri, maumivu mesharabu
Libichi lichirichiri, lanyekenya, lajilabu
Hatiwa moto sumari, ati tiba mjarrabu
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto
Sumari moshi lafuka, kwenye donda likatiwa
Donda lilivyochemka, wamba kwapwazwa maziwa
Na huku wao wacheka, “sasa donda litapoa”
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto
Vidudu vyaangamizwa, donda visiliadhibu
Kumbe huku naumizwa, maumivu ya ajabu
Kwa kweli ningesikizwa, ‘ngegomea matibabu
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto
Sumari linalowaka, nimeshachomwa dondani
Na maumivu hakika, bado yapo si utani
Mbele ya watu nacheka, wanone ni afwani
Ni tiba ya donda bichi kutiwa sumari moto
Donda hili kutibika, si rahisi asilani
Kila saa na dakika, natonesheka kwa ndani
Nje hukaa hacheka, halia nikiwa ndani
Donda tatizole kuu, ni mwiba uliongia
Mwiba wa nyenga mkuu, alopea na kupea
Na sitapata nafuu, kwa namna ulivyongia
Ulichoma ukapinda, ukakaa kama lamu
Kijipande kikaganda, kwenye mshipa wa damu
Ndiyo mana hili donda, kupona haswa ni ngumu
Na kwa tiba ya sumari, nazidi kuteketea
Sumari l-ahmari, kwa moto ‘livyokolea
Nachokorwa kwirikwiri, naona naangamia
Dawa ni kumshukuru, mola wa hii dunia
Kuleta stighfaru, nisije nikapotea
Hii ni yake qadaru, aliyonichagulia
Alhamdulillah, Alhamdulillah, Alhamdulillah
Astaghfirullah, Astaghfirullah, Astaghfirullah
Allahumma ajirnii fii muswiibaty, wakhluf lii khayran minhaa…
Salma Hamad
21 Machi 2013
Zanzibar
Huruma nakuonea. Ila la kufanya sina
Juhudi meziendea. Donda kutaka lipona
Dawa zote metumia. Hadi dua kwa rabbana
Ila lililobakia. Usiache kutafuta
Tiba kuziulizia. Huenda ukaja pata
Ingawa yako kadhia.tiba zote umepita
Usijekata tamaa. Kimya ukajikalia
Hakuna mbaya kadhi. Kwa mola ikakomaa
Maradhi tuliletewa. Meambatanishwa na dawa