KISWAHILI KINA WENYEWE

Mama si Mla Vitamu

Ama ukiwa bibiye, mambo yote bam bam
Kitu gani usikiye, kisikupandishe hamu
Utalitamani biye, hata uambiwe sumu
Ukishaitwa mameye, hudiriki kula tamu

Ama ukiwa bibiye, havishi visingizio
Leo pika bwana weye, mi naumwa n’shikio
Kesho vyereje na weye, ondoka na mihogoyo
Ngoja ta uwe mameye, litakatika hashuo

Ama ukiwa bibiye, mume hamna hasama
Awe ndiye awe siye, weye hutizami nyuma
Siku uwapo mameye, hupatipo tena wema
Ukishaitwa mameye, mapenzi nusu yahama

Bwana aweza jituta, kumfurahisha mke
Katongoa “leo tuta, mke wangu usipike
“Kitakuja kishapikwa, mule na muburudike”
Ela aliye mameye, hadiriki kula tamu

Bwana atafanyafanya, alekee hotelini
Mabega kayakusanya, moja juu moja chini
Arudi na kinying’inya, cha wali wa biryani
Atamba huku akenya, “kula na watoto ndani”

Mamengwa akipokea, kwanza aanza na guno
Kifuko akifungua, afuatizia shonyo
“Bwana huyu augua? Humu sioni mafanyo”
Sasa kashakuwa, mama hadiriki kula tamu

Mame ende kwa jirani, polepole si kwa zogo
“Jamaa mumpikani, munitilie kidogo
Nitawapa biriyani, munigaie muhogo”
Si kwamba autamani, umamengwa ni mzigo

Roho yake yamsubu, aitaka biriyani
Ela ‘kipiga hisabu, ale nani aache nani
Ndipo apatapo jibu, la kugonga kwa jirani
Ubibiye ushaghibu, mama tamu ni ya nini!?

Hapo vianze vijembe, akishakaa pembeni
Bwana huyu kwa upambe, ndio aambiwe nini
Angalinunua pembe, lingetuchawanya ndani
Ama aitwae mama, hadiriki kula tamu

Beti hizi zinatosha, siendi tena usoni
Nnangia sehodisha, nawaomba samahani
Musijeni nifurusha, neghumiwa ikhiwani
Na nyie mungechekecha, mutaona kama mimi?
Ati aitwae mama, adiriki kula tamu?

Salma Hamad
21 Februari 2013
Zanzibar

1 thought on “Mama si Mla Vitamu”

  1. Tamu ndivyo adiriki, kuila kiitamani,
    Ila yataka wafiki, mapenzi yasobinywani,
    Ampatae wa dhiki, faraja kimuwazani,
    Hetayona tofauti, kila siku yu penzini,
    Ila hivi ni kufundwa, tokea yumtotoni,
    Kwavyo inawezekana!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.