KISWAHILI KINA WENYEWE

Sistahiki Lalama

Rabbi ‘menipa uzima, wa mwili na wa akili
Bila maombi kutuma, andishi wala kauli
Waniachia nahema, silipi senti mbili
Sistahiki lalama, miongoni mwa wajawo

Menitunuku elimu, ya dunia na akhera
Ukanipa uisilamu, iwe ndio yangu dira
Sina cha kukulaumu,Rabbi Rahimu Ghafura
Mimi si wa kulalama, miongoni mwa wajawo

Mola umenipa mke, kama nilivyomtaka
Mke mwenye sifa zake, za umbile na khuluka
Yuaniridhi kwa yote, anipa nnachotaka
Sina haki kulalama, miongoni mwa wajawo

Meniruzuku na wana, kwa jaalayo ya Rabbi
Yasmin na Zuwena, wazuri wamaridadi
Wanipa furaha sana, moyo uradhi baridi
Sithubutu kulalama, miongoni mwa wajawo

‘Menichagulia mama, nisitake mwenginewe
Mja wako bi Zuwena, sijaona mfanowe
Na ndugu kyemvu kizima, kwani usishukuriwe?
Ama siwezi lalama, miongoni mwa wajawo

Ni mengi uliyonipa, idadi siikariri
Hadhi ukanipandisha, kwa utungo wa hariri
Ukitaka wanipoka, bila ya langu shauri
Tena vipi nilalame, miongoni mwa wajawo?

Bila ya Wewe kutaka, mimi siwezi chochote
Siwezi hata kupwesa, hata kuinua kope
Ndio mana najiasa, nikushukuru kwa yote
Si mimi wa kulalama, miongoni mwa wajawo

Hamad Hamad
18 Februari 2013
Copenhagen

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.