Leo siku imefika, ya huzuni kutungia
Chozi halitakauka, Nyoyo zimejinamia
Bachu ameshatutoka, enda huko kwa jalia
Leo yametimilia, ya dhaaikatul mauti
Nasi tuliobakia, twausubiri wakati
Wetu hatujaujua, mchana ni lailati?
Umepigana hakika, Bachu, dini kuwa juu
Yakakukuta mashaka, na jeuri za wakuu
Hwekubali tetereka, Bachu, ni kidume mji huu
Yote ulotufundisha, twayatia matendoni
Kusudi kukamilisha, kazi yako ya mwanzoni
Japo dola yatutisha, yatuweka vifungoni
Ewe mola maulana, mpokee mja wako
Mpe kila la kufana, mjaze rehema zako
Mnyanyue juu sana, awe kwa wapendwa wako
Said O. Shoka
13 Februari 2013
Zanzibar