Zenji yetu yatoweka, yatoweka naiona
Ndio ndoto nnoota, usiku hata mchana
Ndoto hii yanifata, nendako yaniandama
Siamini nnoota, sitamani kuyaona
Naota kila kukicha, habari huwa nasoma
Mitandaoni napita, yalojiri kuyaona
Zenji nyumbani kwapwita, shuari haiko tena
Kuchafu kumechafuka, si shuari si salama
Bahari inachafuka, naota meli zazama
Roho zinapukutika, mikondoni zinkwama
Walio juu wacheka, hiyo kwao ni neema
Na waliosababisha, habari hata hawana
Makasri ya shubaka, yalojengwa kwa gharama
Yaloipatia sifa, Zenji dunia nzima
Naota yaporomoka, mengine ngoda yanama
Taratibu yanyofoka, naota Zenji si njema
Naota mwitu wawaka, joto hilo laririma
Jozani yayayatika, joshi juu laparama
Faya zipo zishafika, moto haziwezi zima
Mbuga, wanyama na nyika, ma’lesh havipo tena
Naota watu wabweka, wabwekea wao wana
Wana wanapoinuka, kutoa chao kyalima
Kupinga wasichotaka, kwa chema wanachoona
Wana kiapo ‘meapa, n’go hawarudi nyuma
Nayaota makanisa, yanajaa isilama
Misikiti yafurika, kiristu mejazana
Kila mtu kajiweka, pasipo pake kwa jina
Mambo yamechanganyika, naona vyangu nakama
Mnadani yanadishwa, nchi hivi naiona
Madalali wana hisa, bei wapunguziana
Naona mwisho shafika, Zenji hiyo yayoyoma
Sekunde zahisabika, Zenji haiyetu tena
Nakataa kuamka, bora nilale daima
Niendelee kuota, yasijiri niloyona
Kwa maana hiamka, tashindwa kulala tena
Nalala sebu amka, ukweli sebu uona
Hamad Hamad
12 Februari 2013
Copenhagen
Kwaheri zanzibar
Ahsante Hamad Hamad
Tunakushukuru kwa kutupatia mawaidha kwa njia ya burudani ya asili ya kizanzibari.
Mimi nafikir jibu tunalo.ila naamin Mungu yupo.na hakubali waja wake wadhulumiwe hasa waco na hatia.shair zuri lina maana.
Ni kweli kabisa uyasemayo, zanzibar inaingia katika mkondo mkubwa kwa majanga mbali mbali yanayoikumba.
Sadakta Hamad,