Sauti yanikauka, kuililia watani
Machozi yapukutika, pukupuku mashavuni
Kifua chatatalika, chakatikia kwa ndani
Kwa kulilia watani
Dola iloimarika, ndivyo ‘likuwa zamani
Mashariki afrika, kusiwe na mpinzani
Wageni wakavutika, kuja weka maskani
Sasa iwapi watani
Wageni walivutika, kuja weka maskani
Walitoka Amerika, Uchina na Arabuni
Wahindi na Sri Lanka, Zenji pakawa nyumbani
Nansononeka watani
Watani nasononeka, hikuona hilakini
Mamlakayo kupokwa, ukawa huna hunani
Na watuwo wateseka, kukimbia watamani
Huzuni kubwa watani
Watu wako wateseka, kuhajiri watamani
Majumba yaporomoka, hakuna wa kuyahami
Walopewa madaraka, yaishia matumboni
Yasikitisha watani
Walopewa madaraka, kutwa wamo vikaoni
Kujitia hangaika, na kujivisha huzuni
Kubwa wanalolitaka, waonekwe tiviini
Si kwa shidazo watani
Meli zinapopinduka, tasikia hotubani
“Sote tunasikitika, kwa hii kubwa huzuni”
Mapesa yakachangishwa, kwa jina la masikini
Watu wako ya watani
Mapesa huyachangisha, kutoka nje na ndani
Mabilioni ya pesa, yakaishia hewani
Watuwo waathirika, ‘kaambulia vipeni
Tadhlili ya watani
Watuwo wadhalilika, wanotaka kukuhami
Magerezani kuswekwa, na kuitwa mahaini
Kosa kubwa walitaka, hadhi yako ya zamani
Hawajatoka watani
Ni mengi yanofanyika, ya dhuluma ya watani
Zenji ishafisidika, dhulma ndio sukani
Yote ningeyaandika, ningeweza natamani
Ila siwezi watani
Hamad Hamad
28 Januari 2013-01-28
Copenhagen
Asante Bwana hamad, kwa kweli hapo umetulia na kutukumbusha nyumbani kwa maneno yako ya busara ktk hali ya ushairi, mashairi imekuwa ni vitu ghali sasa na wengi hawapendi tena kuendeleza utamaduni huu yaliyobakia leo ni zenji fleva ambayo hata hupati mantiki yake yakoje. Ni mategemeo yangu tutakuwa pamoja nawe katika siku za baadae INSHAALLAH.
Waache watakaburi, uongozi una mwisho.
Hawa hawatafakari, Salmini hana macho.
Alojifanya jeuri, leo ana mkong’oto.
Kaacha kimurimuri, Komando kawa mtoto.
Hana tena ujabari, anakiona cha moto……
Komando kawa mtoto, kwa dua za watu wake.
Aonja ladha ya moto, kabla ya kifo chake.
Mungu mzidishe joto, uwazindue wenzake.
Uchochee wake moto, ahisi ndotoni kwake.
Aharishe kwa kokoto, iwe funzo kwa wenzake……
Wamezoea dhuluma, hata hisia hawana.
Wamesahau kuhama, Ikulu pia Madema.
Lolote kwao kufanya, ndio yao sunna njema.
Ati hujua kusema, Inaf ndo sera njema.
Kitasimama kiama, waende kusema tena…….
Tunataka nchi yetu, kwanini hamfahamu.?
Zanzibar sote ni yetu, sote tunalo jukumu.
Sijifanye watukutu, mkajitoa fahamu.
Kwanini hamna utu, ni kama wendawazimu.
Hatutocmama katu, na hilo mlifahamu……
Mcjifanye samaki, kwa kuzidi ujabari.
Mkaisahau haki, sababu vimurimuri.
Wameshapita lukuki, ziko wapi zao mori.?
Nchi yetu itabaki, na jina la Zanzibari.
Hata kama hamtaki, hio ndo kwenu habari…….
Hongera mshairi lkn inatia huzuni saaaana kukpsa utaifa
safi kabisa nimeipenda sana nakupongeza sana.
Hapo wajina umenimaliza Wape vitu vyao lakini sikio la kufa halina dawa