Kucheza tucheze kwetu, kwetu tulikozaliwa
Kunako wazazi wetu, wazazi waheshimiwa
Heshima asili yetu, tuiombe tutapewa
Vijana tucheze shime, hima tutaaminiwa
Tucheze kike kiume, hamna kubaguliwa
Tucheze tusisimame, mchezo hautakuwa
Tucheze tufanye ari, tukijua tutapewa
Tuzipandishe na mori, na kwa nguvu tulizopewa
Wazee wakitukiri, zawadi tutachukuwa
Hili halina ubishi, kwetu tukikuchaguwa
Kwazidisha ushawishi, mchezo tukanogewa
Kwetu michezo haishi, kila tutapoamua
Nasisitiza kwa leo, na maneno kufungiwa
Hajuti mcheza kwao, hata akikosolewa
Anayo mapendeleo, kila mchezo ukiwa
Said O. Shoka
19 Januari 2013
Zanzibar