Mweledi wa tabasamu, hebu nitabasamiye
Uniondoshee ghamu, moyo wangu utuliye
Lako wewe ni adimu, sijaona mfanowe
Fumbua midomo yako, iachie ‘sishikane
Niuone mnenepo, wa vishavuvyo vinene
Na kwa ndani mpasuko, wa mwanyao niuone
Na puayo ya upanga, vile inavyonyooka
Ikafanya ncha changa, kudasa yatamanisha
Mchanganyo wa kimanga, na asili Afrika
Na kwa machoyo laini, yanayofura mapenzi
Yenye umbo wastani, la jani la m’baazi
Hayakaipo huzuni, bashasha ndo’ yake vazi
Tabasamu e mwandani, nami uniambukize
Nitabasamu kwa ndani, na nje lijitokeze
Tabasamu la thamani, hadhiye usiibeze
Hamad Hamad
17 Januari 2013
Copenhagen