Nealikwa watuningwa, kwenda kusherehekea
Sherehe ya mwaka mpya, huu ulioingia
Hafikwa ni ya kufikwa, hapa tawasimulia
Kwewa na kila namna, ya vyakula na kunywiwa
Vya Kizungu na Kichina, vya kuchotwa na kubwiwa
Nikala bila khiyana, nikashiba havimbiwa
Kituko kikaja tuka, pale tulipoambiwa
Ifikapo saa sita, kinywaji tutapatiwa
Kinywaji kisicho shaka, si kilevi haambiwa
Ingawa newa na shaka, kuamini haamuwa
Kwa kuwa alonalika, ni mtu namuelewa
Kiovu hawezi nipa, hathubutupo najua
Moyo ukaja nirapa, shampeni kugunduwa
Nikajawa ni wahaka, ela siweze kimbia
Saa sita ikafika, chupa tukasogezewa
Huku nje kwaalika, fashfashi zin’jaa
Kinywaji chamiminika, gilasini kwa madaha
Chan’gara chameremeta, bilauri haitwaa
Kwa shaka na kuogopa, ndogo ndogo hachubuwa
Kinywaji kikanipata, hajiona nanogewa
Nikanywa bila kusita, gilasi haikubwia
Bada kitambo kupita, domo likaanza pwaya
Mipweso napwesa pwesa, macho siwezi fumbuwa
Mara macho yarembusha, kwa juu yalewalewa
Mwenyeji namtafuta, aje nipate mwambiya
Haya yaliyonikuta, apate nisaidiya
Niaminivyo naota, au jamaa nshalewa?
Hamad Hamad
1 Januari 2013
Copenhagen
Kake weye kunlewa kushalewa muungwana
usije ukanogewa ukaja kulewa tena
Ila utasamehewa ukimuomba rabana.
Weonaje kake yangu mvinyo ulipopiga
Hivi ladhaye ni chungu au ni kama ya togwa
wepatikana mwezangu wazungu walikutega
kake usionje tena tutenda kunywa peponi
ladha za kila namna na Mahur l Eini
kake ukionja tena hwendikunywa wa peponi
Nakwambia kabisaaaa!
Ndugu yangu kunlewa, pole kwa kujisifia.
Wenzako washakuoa, ndivyo walivyozoea.
Jua washakubirua, bilisi achekelea.
Na nguo washakuvua, wenyewe kujilipia.
Walikutaka zamani, kukwambia ni vigumu.
Uliona ihsani, kukupa vilo vitamu.
Watu hawana imani, kote wameshakuchumu.
Washakutia chumbani, na kuja zamu kwa zamu.
Ulifataje ya watu, ewe mpemba mwenzangu.
Umesahau ya kwetu, ya Wete na ya Madugu.
Mwaka mpya si wa kwetu, tuwaachie wazungu.
Sisi tunao wa kwetu, alotupangia Mungu.
Uliona shampeni, kwa nini ulijinywea?
Ukajifanya muhuni, ushamba kuukimibia.
Sasa mavi yako chini, na yai ushabanjiwa.
Lawama zende kwa nani? mwenyewe wejitakia.
Wajidanganya ni ndoto, kujifanya hufahamu.
Na kutufanya watoto, tuna akili timamu.
Wewe sasa ni mtoto, kwa ulowapa utamu.
Na huna hata majuto, wahadithi bila gamu.
Weacha ya kuhadithi, wasimulia ya pombe.
Hayo ndo tuloyarithi?, kwa wavyele na vikongwe?
Usijitie nuhusi, maisha usiyazonge
Sisi kwetu ni matusi, kuvishiriki vigenge.
Kwanini sishereheke, kwa mwaka wa hijiria?
Naamini siku yake, pengine hukuijua.
Hujui maana yake, hata ilivyoanzia.
Hala hala ewe kake, pole kwa kutojijua.
Tambua sipo ulipo, wafanya usoyajua
Usifuate upepo, ukazidi kupotea
Tubia hapo ulipo, Allah anakungojea.
Akulipe yake pepo, jirani na manabia.
By: Al’Rumhy.