Kuna yule ajuae, na ajua yuajua
Tatizo mpelekee, lolote atatatua
Yuajijua mwenyewe, kwamba yeye yuajua
Kuwa karibu na yeye, elimuye kuchukua
Mwengine ni ajuae, na hajui yuajua
Elimu i tele naye, hana asichokijua
Ela aonavyo yeye, yu juha wa kurembewa
Huyu na ashituliwe, hadhi yake kuijua
Na kuna asiyejua, na ajijua hajui
Mambongwa huyakimbia, watuni yeye hakai
Adhara aichelea, kuja tolewa nishai
Huyu si wa kuzomewa, ni wa kufunzwa kwa rai
Wa nne ni asojua, na hajijui hajui
’kiitwa kuhutubia, himahima hakatai
Maringo kujisifia, yukajifanya nabii
Huyu ni kushushuliwa, yukaambiwa hajui
Wa kwanza ni ajue, akajua yuajua
Wa pili ni ajuae, na asijue ajua
Wa tatu ni asojua, akajijua hajui
Wa nne ni asojua, yusijijue hajui
Hamad Hamad
25 Disemba 2012
Copenhagen
Wako wengi wanojua, wenyewe hujifahamu.
Hao mengi huyajua, yeyote humuheshimu.
Popote hujitambua, huongozwa na elimu.
Mwengine nae hujua, bila ya kujifahamu.
Yale anayoyajua, yote ni mambo muhimu.
Aje wa kumzindua, watu wachote elimu.
Wa tatu ni asojua, mwenyewe hujifahamu.
Hupenda nae kujua, tena kwa zote nidhamu.
Yafaa kumpokea, kumpa yenu elimu.
Wa mwisho ni asojua, na kujiona Mwalimu.
Hana analolijua hata, kushika kalamu.
Huyu huungua jua, sawa na mwendawazimu.