Nikuwinde hadi lini, niipate salamuyo
Wanikimbiya kwa nini, kunifanyia uchoyo
Wajua nimapenzini, utosi hadi unyayo
Ndio ukatenda hayo
Ningojee hadi lini, kuuona wajihiwo
Wajikimbiza gizani, waruka huna kituo
Hikuuliza kwa nini, wanamba nitabiayo
Wanijua taumiya
Wataka nifanye nini, niipate kauliyo
Unambiye ukenami, nami nipate pumuo
Nga’ hiuzwa n’waani, n’jidai mmaliyo
Sininyime nitakayo
Hamad Hamad
21 Disemba 2012
Copenhagen
mwenye kutaka hachoki, kaza kamba ndugu yangu
kuwinda ni mikakati, si nguvu zitumikazo
winda ja kama hutaki, taja mwenyewe kwa mbio
ukichoka ushapata
Ndugu yangu si pekeyo, mfano wako ni wengi.
Yashanikuta mwenzio, hetaka kuvuta bangi.
Nilianzaia Bweleo, nikafika hadi Nungwi.
Sababu mtoto huyo, nampenda hanipendi.
Kwanini?
Kwanini najiuliza, sababu yake sioni.
Azidi kunitatiza, hanitoki mawazoni.
Kila nikimuuliza, anikataa kwa nini?
Ashindwa kujieleza, ni kama hana ulimi.
Nashangaa..!
Nashangaa akipita, namuuliza hasemi.
Chochote anachotaka, akitaje kwangu mimi.
Penzi lake kulikosa, kwangu ni umasikini.
Kwangu hataki kuckeka, tabasamu silioni.
Nisaidieni…..
Nisaidieni nyote, kwa rai na kwa hekima.
Huyu binti nimpate, niwe Baba awe Mama.
Mawazo nipumzike, mwenzenu mechoka sana.
Niliseme jina lake? mupate kumuandama?
Naumia..
Naumia si utani, homa gonjwa la kitoto.
Mapenzi yapo moyoni, anijia kwenye ndoto.
Natamani afueni, nipoe na hili joto.
Kwa vilivyo duniani, huyu kwangu ndio pepo.