Habari za uchawini ndotoni zilinijia
Kubwa zisizo kifani ndugu yangu nakwambia
Ndugu yangu wa imani nawe nakudokezea
Uchawini kuna mambo!
Wachawi mahayawani tena ni watu wabaya
Hawana chembe imani na wala hawana haya
Matendo ya kishetani ndiyo waliozowea
Uchawini kuna mambo!
Hawamuogopi Mungu wachawi nakuambia
Wanaua kwa marungu mapanga na majambia
Hata uone uchungu mwiko kukuhurumia
Uchawini kuna mambo!
Mtu huchinjwa shingoni kisu kikamuingia
Damu yaruka hewani wengine washangiria
Si hadithi za kubuni ni mambo yanatokea
Uchawini kuna mambo!
Wanacheza ngoma zao kama walivyozaliwa
Watoto na mama zao wakwe na shemegi pia
Zaimeruka nyuso zao haya zimewapotea
Uchawini kuna mambo!
Suleiman Hakum
16 Disemba 2012
Zanzibar
Ya mchawi huyaoni kama na wewe hujawa
ndugu yetu selemani mbona unatushtuwa
kama kweli ni ndotoni radhi zako tapewa
Uchawini nawe umo?
Lo! kake mie simo simo mie uchawini
Siningize kwenye shimo la wenyeji wa motoni
kama huamini simo naweza kula yamini
uchawini mie simo.
bila kungia ngomani, mchezowe huujui
kama huli uchawini, kamwe hututongolei
siri nzito jamani, nani kakutobolei?
au ulialikwa?
Nami nimepata shaka,maneno ulotwambia,
Umeningia wahaka,sijui pakuanzia,
Kwa jina sinamashaka,na njema yako tabia,
lakini sijaridhika,vipi weyajuwa haya?
Somo kwani nawe umo, He tuweke bayana
Ungalimo kwenye shimo, Tueleze kwa mapana
Uchawi kwani ni shimo, Lilo refu tena pana
Tuwekaneni Bayana.
Taireni taireni , mbona mwanielemea
Hayo mambo ya ndotoni , si nilishawambia
Mimi simo uchawini , ndugu zangu nawambia
Uchawini mie simo
Seleman hana kosa. Hili aliloongea
Ni wangapi ‘mewakosa. Rafiki zeti wekuwa
Wachawi wakajitosa. Nyama wakenda jilia
Wangapi mechuliwa. Kisha kwetu kurejea
Lengo lao kuwatowa. Vituko kuwafanyia
Kisha tunahadithiwa. Ya huko yanotokea
Jamani seleni yuko sawaaaaaaaaaaa
burudani hapa kweli kweli mimi sijuwi kunena
Wa Hakumu nakwelewa, ndoto liyojiotea,
Wachawi twavyoambiwa, ndotoni wanatujia,
Warambisha, wakwangiwa, waburuzwa jionea,
Kwavyo siyo yako hoja!
Pamoja kutwaambia, ndotoni mejionea,
Sisi twaona vioja, kamwe haiwezi kua,
Uote bila ya haja, lazima wejiendea,
Twambe kama ushingia!
Wallahi sijaingia , naona mwanionea
mbona mnanichangia , kutaka kuniumbua
ndoto ilyonijia , nikosa kuwaambia
Sina nia ya kungia
Haya uliyoeleza. Seleman uko sawa
Hawa wanaokubeza. Juwa hawjaelewa
Mwanzo ulipolianza. Shairi kulitohowa
Tukatae tukubali. Jamani uchawi upo
Hili nasema ukweli.tena nakula kiapo
Tena una mafahali.popote pale wendapo
Alonena selemani. Hakika hajakosea
Naomba muyaamini.’Singizini lomjia
Habari za uchawini. Mitaani ‘meenea