Kwa jina la Zanzibari, uhuru tuliupata
Uhuru ulobashiri, Zanzibar kuneemeka
Mwezi wa kumi na mbili, sitini na tatu mwaka
Na UN tukafika
Kwa jina la Zanzibari, uhuru tukaja pokwa
Mapinduzi Januari, ndicho kilichofanyika
Tukanza upya safari, kwenda tusikokutaka
Tukaanza taabika
Kwa jina la Zanzibari, mapinduzi yakatekwa
Kwa mungano uso kheri, Unguja na Tanganyika
Tukawa kama sifuri, nchi iso mamlaka
Ndipo hapa tupo sasa
Kwa jina la Zanzibari, uhuru mpya twataka
Mpya wa kujiamuri, tufanye tunavyotaka
Tusivutwe kwa shemeri, tuwe baidi na nyika
Twataraji tutafika
Kwa jina la Zanzibari
Uhuru tuliupata
Uhuru tukaja pokwa
Mapinduzi yakatekwa
Uhuru mpya twataka
Inshaallah tutaupata
Hamad Hamad
15 Disemba 2012
Copenhagen
1 thought on “Kwa Jinalo Zanzibari”