Ndoto yangu ya awali, ya kutaka uraisi
Sasa n’shaibadili, siuwezi najihisi
Uraisi si akili, si elimu si ukwasi
Siwezi kuwa Raisi
Uraisi ni kiburi, kwa maana yetu sisi
Kufanya watu dhalili, kuwageuza vinyesi
Kuwadhoofisha hali, bila ya hata kisisi
Sitaki kuwa Raisi
Dhuluma huwa sukani, ya kuiendesha nchi
Kuwanyonya masikini, kuwapora zao haki
Kuwatia hatiani, na kuwabambika kesi
Nachelea Uraisi
Uraisi ni khiyana, miadi kuikhalifu
Mwanzoni unoyasema, kwa ulimi mnadhifu
Mwishoni waja yakana, kwa matendoyo machafu
Uraisi si rahisi
Jisahau nachelea, nikija kuwa Raisi
Kutuma watu kuuwa, kupiga na kunajisi
Sababu kubwa kwa kuwa, hawetaka nifuasi
Siutaki uraisi
Kuwa Raisi mwongozwa, sitaki sitadiriki
Sitaki kutumilizwa, ni wasiositahiki
Hawa mbwa hasumizwa, nitende kile na hiki
Siuwebu Uraisi
Nakichelea kiapo, cha kugwia msahafu
Cha kukazanisha macho, hajifanya sina khofu
Nacha pazwa hagwa papo, haja habopwa n’tutu
Kuwani nyie raisi
Hamad Hamad
4 Novemba 2012
Copenhagen