‘Ngekuwa mla hasara, ‘ngeoa kwa uzurio
Hawa mja wa papara, hakona hakupendao
Haikosapo busara, havutiwa uzurio
Leo nakiri ‘ngeyuta, ngeoa kwa uzurio!
Nekumbuka ‘lipokona, mato yalipoangaza
Malaika nekuona, wameta wanchichiza
Hafikiri setaona, alokuzidi aziza
Ningekiona cha moto, ‘ngekuoa kwa uzurio!
Akili libadilika, na moyo ukafatiza
Matozi yebubujika, mtima wauumiza
Henenda hajiapiza, ‘takuoa nikifanza
Ela leo nakubali, ‘ngekuwa mla hasara!
Usia ulotolewa, wazazi walonifunza
Mwanamke kuolewa, kwa tabia ni aziza
Si sura wala si quwa, si ukoo unojuza
‘Ngewakana ningeyuta, mayuto ya milenia!
Basi lipokumbukia, wasia niloagizwa
Nekaanza kukwambia, nawe kiona wavizwa
Hasira ukatukua, na maneno yasofunzwa
Ela ningelazimisha, leo ‘ngekuwa tabuni!
Dini mafunzo hubiri, kwa mchumba kumwegeza
Mwili wake usitiri, na ngoma asijecheza
Papo ugomvi shamiri, na matusi kichombezwa
Wazazi walinipenda, ‘tawashukuru daima
Moyo ulipata tabu, kuyawacha yalopendwa
Hauasa sijesibu, kujidhuru sijetendwa
Si bora kujisulubu, kwa mashaka yasoinda
Leo unanipongeza, na raha wejionea!
Hawamba wangu mtima, hawamba nisijependa
Huyu kwangu sio mwema, ni bora nimwache kwenda
Nipate mwenye heshima, na dini anayependa
Leo najishukuria, malengo yenfikiwa!
Baada kuusakama, mwisho moyo nikubali
Ukinambia kwa wema, nitafute anojali
Tena nioe kwa shima, nikae nae mithali
Papo hajitafutia, mke nilonae sasa!
Sitara niitakayo, na heshima yangu nyumba
Upole wa lisaniyo, akubali ya Muumba
Tabia njema utuyo, “Hawaa” jina loumbwa
Huyu ndie mke wangu, namshukuru Muumba!
Sitaki tena mwengine, wangu mtima tibua
Sitaki sheti niseme, niwambie wasojua
Sitaki msijipime, kwangu ‘taka jirejea
Nimesharidhika kwake, kwamwe mwengine simwebu!
Othman Ali Haji
Zanzibar
24/02/2012