KISWAHILI KINA WENYEWE

Majina yenye wingi na au kundi zaidi ya moja

Kuna idadi isiyo ndogo ya majina kwenye Kiswahili ambayo huchukua maumbile na makundi tafauti. Miongoni mwa sababu ni kuwa aidha majina hayo yanawakilisha maana tafauti licha ya kuwa na umbile moja, ama ni majina yanayofanana kwa herufi zake lakini tafauti kwenye matamshi na hivyo makundi na, au, ni majina yanayowakilisha dhana moja lakini kwa viwango tafauti. Mada ya leo inazungumzia suala hilo.

Jina moja, maana tafauti

Kwa mfano, jina kifaru kwenye Kiswahili lina maana mbili: ya kwanza ni mnyama wa mwituni na ya pili aina ya gari ya kivita. Jina hili linapomaanisha mnyama, basi kundi lake ni YU-A-WA; na linapomaanisha aina ya gari ya kivita, basi kundi lake huwa KI-VI. Lakini katika makundi yote mawili, wingi na umoja wake hubakia kuwa ule ule: kifaru – vifaru. Tukiyaweka maelezo haya kwenye sentensi, tutapata:

  1. Kifaru kama YU-A-WA
    a. Kifaru amewashambulia wanakijiji.
    b. Vifaru wamewashambulia wanakijiji.
  2. Kifaru kama KI-VI
    a. Kifaru cha jeshi kimeshawambulia waasi.
    b. Vifaru vya jeshi vimeshawambulia waasi.

Majina mengine yenye tabia hii ni kama vile ndege, ambalo likitumika kuwakilisha kiumbe huwa ni kwa kundi la YU-A-WA na likitumika kuwakilisha chombo cha usafiri wa angani huwa kwa kundi la I-ZI.

Maana moja, viwango tafauti

Majina mengine huwakilisha maana ile ile lakini katika viwango tafauti. Kwa jina ‘gari’ linaweza kuwa kwenye kundi la I-ZI, hivyo umoja na wingi wake ni gari – gari, au linaweza kuwa kwenye kundi la LI-YA na hivyo umoja na wingi wake ukawa gari – magari. Tukiweka maelezo haya kwenye sentensi, matokeo yake yatakuwa haya:

  1. Gari katika I-ZI
    a. Gari yangu imeharibika.
    b. Gari zangu zimeharibika.
  • Gari kama LI-YA
    a. Gari langu limeharibika
    b. Magari yangu yameharibika.

  • Majina mengine yenye tabia hii ni kama vile shati ambayo inaweya kuwa kwa kundi la I-ZI (shati – shati) na au LI-YA (shati – mashati).

    Herufi moja, matamshi tafauti

    Kuna majina kwenye Kiswahili yanayofanana kwa herufi zake, lakini tafauti katika matamshi na hivyo pia maana na makundi.

    Kwa mfano, jina paa linapotamkwa kwa p iliyokazwa kwa nje, humaanisha mnyama. Hivyo umoja na wingi wake huwa hivyo hivyo paa na kundi lake huwa YU-A-WA. Lakini inapotamkwa kwa p iliyolegezwa kwa ndani, humaanisha sehemu ya juu inayofunika nyumba, na hivyo wingi wake huwa mapaa na kundi lake ni LI-YA.

    Tukiyaweka maelezo haya kwenye sentensi, tutaona kuwa:

    1. Paa kama YU-A-WA
      a. Paa anafukuzwa na chui.
      b. Paa wanafukuzwa na chui.
  • Paa kama LI-YA
    a. Paa la nyumba limeezuka kwa upepo.
    b. Mapaa ya nyumba yameezuka kwa upepo.

  • Maneno mengine yanayoingia kwenye kigawe hiki ni kama vile kaa, ambalo linapomaanisha mnyama wa pwani huwa na kundi la YU-A-WA na, hivyo, kuwa na wingi wa kaa, na likimaanisha kaa la moto huwa na LI-YA, na hivyo na wingi wa makaa.

    Jina moja, wingi tafauti

    Watumiaji wa lugha wanatafautiana katika majina yanayowakilisha watu wa karibu kifamilia na kimahusiano. Majina hayo ni kama vile mama, baba, kaka, dada, babu,  bibi, shangazi, ami, khaloo, shemegi na rafiki.

    Wengine huyatumbukiza kwenye kundi la I-ZI na hivyo umoja na wingi wake haubadiliki, yaani wingi wa baba ni baba, kwa mfano huu. Wengine, hata hivyo, huyatumbukiza kwenye kundi la LI-YA na hivyo wingi wake huchukuwa kiambishi awali cha ma-, yaani wingi wa babu ni mababu, kwa mfano huu.

    Kwenye sentensi, maelezo haya yatakuwa hivi:

    a. Bibi zangu wananipenda sana.
    b. Mabibi zangu wananipenda sana.

    Mimi nakubaliana na matumizi yote mawili.

    Hata hivyo, sikubaliani na wale wanaolazimisha kwamba majina hayo yabakie na muundo wa majina mengine kwenye kundi la YU-A-WA wa m-wa-. Hao ndio wanaosema mbaba na wababa wakiigiza mwalimu na walimu.

    Hili hapana!

    1 thought on “Majina yenye wingi na au kundi zaidi ya moja”

    Leave a Reply

    Fill in your details below or click an icon to log in:

    WordPress.com Logo

    You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

    Facebook photo

    You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

    Connecting to %s

    This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.