KISWAHILI KINA WENYEWE

Yaliyomo kwenye kundi la YU-A-WA

Sadfa imeyaweka majina yanayonasibishwa na roho (nafsi) kwenye kundi la YU-A-WA, vikiwemo viumbe tunavyoviona – watu, wanyama, ndege na samaki – hadi tunavyoamini kuwapo kwake bila kuviona kama malaika, majini, mashetani au pepo. Wote hao wanaingia kwenye kundi hili. Sadfa pia imefanya hili liwe kundi pekee ambalo hayakutikani majina yasiyo na sifa ya nafsi.

Leo ningelipenda kuzungumzia namna pande mbili za YU- na A- kwenye kundi hili YU-A-WA zinavyotafautiana kimuundo. Na kama kawaida, kuzungumza kwa mifano huwa kunairahisisha kazi. Angalia mifano hii katika umoja:

  1. Mtoto wangu huyu mmoja bado ni mdogo.
  2. Dada yangu huyu mmoja bado hajaolewa.

Halafu tuziandike tena sentensi hizo hizo kwa wingi:

  1. Watoto wangu hawa wawili bado ni wadogo
  2. Dada zangu hawa wawili bado hawajaolewa.

Je, umeona kitu gani cha mfanano na mpishano?

Bila ya shaka umeona mfanano katika vioneshi vya karibu (huyu, hawa) na vivumishi vya nambari (mmoja, wawili). Lakini umeona mpishano katika sura za majina yenyewe – mtoto katika wingi ni watoto lakini dada inabakia kuwa dada sio wadada. Umeona pia mpishano katika kivumishi cha kumiliki kwenye -angu: mtoto/watoto wangu ila dada yangu/zangu.

Ilipoingia YU-

Ni sababu hii ndiyo iliyofanya kundi hili kupewa jina la YU-A-WA na wasomi wa lugha. Hiyo YU- imewekwa kuwakilisha kiambishi kinachowakilisha yale majina yanayotumia muundo huo, mfano dada, kaka, mama, baba, bibi, babu, shangazi, rafiki, wifi, shemegi, ami, khaloo, n.k.

Majina haya yana muundo wa pekee kwa sababu yanachukuwa sura na tabia za yale majina ya kundi la I-ZI kwenye umbile la umoja na wingi, ambapo vyote huwa na sura moja, na pia katika vivumishi vya umilikishi. Lakini yanabeba  tabia za A-WA kwenye vivumishi vyengine na aina nyengine za maneno ndani ya sentensi.

Kwa mfano, katika kikundi cha maneno “Kaka yangu huyu mmoja” kivumishi yangu kimefuata muundo wa I-ZI, lakini vivumishi huyu na mmoja vimefuata muundo wa A-WA. Ingelikuwa kikundi chote cha maneno kimefuata muundo wa I-ZI, basi kingelikuwa: “Kaka yangu hii moja” au kama chote kizima kingelifuata muundo wa A-WA, basi kingelikuwa: “Kaka wangu huyu mmoja”.

Wingi wa Kaka ni Kaka, Makaka au Wakaka?

Ninatambua kwamba kuna baadhi ya watumiaji wa Kiswahili huufanya wingi wa majina niliyoyataja hapo juu kwa kuongeza kiambishi ma- kama madada, makaka, marafiki, mabibi, mababu, na kadhalika. Ninatambua pia kuwa kuna wanaosema mdada – wadada, mkaka – wakaka na kadhalika.Kwa hapa ninataja tu kutambua kwangu. Katika mada inayofuata ya “Majina Yenye Wingi na Makundi Zaidi ya Moja” nitafafanua msimamo wangu.

Sura Mbalimbali za A-WA

Tumalizie na sura mbalimbali ambazo majina kwenye kundi hili hujitokeza kupitia sehemu ya A-WA. Nazifahamu sura tano:

  1. Sura ya M-Wa kama ilivyo kwenye mtoto – watoto
  2. Sura ya ()-Ma kama ilivyo kwenye daktari – madaktari
  3. Sura ya Ma-Ma kama ilivyo kwenye malaika – malaika
  4. Sura ya () – () kama ilivyo kwenye samaki – samaki
  5. Sura ya Ki-Vi kama ilivyo kwenye kijana – vijana

Jambo la msingi ni kuwa sura zote hizi tano kwenye sehemu ya A-WA katika kundi hili la YU-A-WA zinafuata aina moja ya upatanisho wa kisarufi, yaani uhusiano baina ya jina na aina nyengine za maneno ndani ya sentensi. Tafauti na ile sehemu ya YU- tuliyoifafanua mwanzoni.

4 thoughts on “Yaliyomo kwenye kundi la YU-A-WA”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.