Bada ya vyote kutwaa, ukavifanya ni vyako
Ukaviba kwa hadaa, vikawa miliki yako
Bado ukegaagaa, wataka ramba na mwiko?
Fisadi usotosheka, likutoshalo n’dongo
Pya kunnikukuta, sina kilichonibaki
Si nkuti si wa shuka, si mzima si maiti
Sasa nakwamba kopoka, utakalo hulipati
Likutoshalo n’dongo, fisadi usotosheka
Wenda dai uongezwe, yawe mbali masafayo
Kwangu miye kupunguzwe, nibakwi maji ya nyayo
Kwako kuje kujalizwe, ufurahike rohoyo
Unyanda hausogezwe, palipo ndipo kituo
Kwa husuda ulonayo, hakuna pakutoshapo
Duniya iwe maliyo, utamba mpa na hapo
Ela naiji siriyo, itabaki kuwa ndoto
Kitachosinza kiyuyo, ni dongo peke na moto
Hamad Hamad
20 Januari 2012
Copenhagen