Ukweli utakaobakia daima ni kwamba lugha ni sauti za nasibu. Hili haliwezi kupingika. Ukweli unaoweza kuzua ubishani ni kwamba ndani ya sauti hizo za nasibu muna aina moja au nyengine ya kanuni. Ni kanuni hizi ndizo ambazo wataalamu wa lugha (wanaisimu) hujiaminisha kwamba wanaweza kuzitumia kutoa muongozo wa vipi lugha inapaswa iwe, badala ya kuelezea vile lugha ilivyo. Nisifahamike kuwa nina ugomvi na wasomi wa lugha. Hapana!
Hoja yangu ni rahisi tu wala haiwapingi wasomi wa lugha. Bali inasema kuwa msomi wa lugha awe awavyo, hana jukumu na wala hawezi kutoa muongozo wa vipi lugha itumike kwa wenye lugha hiyo. Kikubwa anachoweza kukifanya, kwa mafanikio kabisa, ni kueleza namna wenye lugha yao wanavyoitumia lugha hiyo.
Hapa nitaulizwa: “Sasa kwani wewe mwenyewe unafanya nini hapa?” Nahisi ninafanya kinyume chake. Ninachofanya ni kuwa sehemu ya kundi la pili: la kueleza vile lugha inavyotumika kwenye jamii ya Waswahili wenyewe, nao ndio walionizaa, kunilea na kunipa lugha niliyonayo. Swali la mwisho nitakaloulizwa: “Kwani hao Waswahili wenyewe ni nani?” Ni wenyeji wa upwa ya Afrika ya Mashariki, ambao Kiswahili ndio lugha yao na Uswahili ndio utambulisho na utamaduni wao. Hawa hawana lugha nyengine ya kuiita yao, hawana mahala pengine pa kupaita pao na wala hawana utambulisho mwengine wa kujiita ni wao. Nami naona fahari ya kuwa mmoja wao. Hili lisichukuliwe, hata hivyo, kwamba ni kutangaza ukubwa na utukufu. Hapana. Mimi ni Mswahili tu. Si zaidi ya hilo.
Dibaji imalizikie hapo. Sasa kwenye mada ya leo juu ya kundi la majina la LI-YA, ambalo kwa mtazamo wangu lina vitendawili na mafumbo yake. Nitazungumza kwa mifano. Katika hali ya jumla-jamala, kiumbile maneno haya yakiwa kwenye wingi wake huwa na kiambishi cha ma- kama majina haya: macho, mawe, masikitiko, maneno, majibu, makabati, matunda. Majina haya, hata hivyo, katika umoja wake hayakufanana. Kwa mfano, umoja wa macho ni jicho kama ulivyo umoja wa mawe kuwa jiwe. Lakini umoja wa maneno ni neno na wa majibu ni jibu.
Kama hujaona tafauti hapo, nitakuonesha. Tafauti ya maumbile ya majina hayo ni kuwa, katika kundi la macho na mawe, umoja wake una kiambishi kimoja cha ji-, lakini hayo mengine lile jina la kwenye umoja huachwa kama lilivyo na likaongezwa kiambishi ma- kulifanya kuwa wingi. Ingelikuwa kanuni ya umoja na wingi inafanana kwa majina yote yaliyomo kwenye kundi la LI-YA, wingi wa jicho ungelikuwa majicho na wa jiwe ukawa majiwe, au kinyume chake basi wingi wa neno ungelikuwa mano, na wa jibu ukawa mabu.
Sijamaliza. Kuna fumbo jengine. Majina mengi kwenye kundi hili hayana umoja bali wingi tu. Majina kama maji, mahitaji, madhumuni, matokeo, maradhi, mashambulizi, mafuriko, maslahi, mabishano, maisha na kadhalika na kadhalika, yote hayana umoja bali yana wingi tu. Mara kadhaa husikia watumiaji wa lugha wakishindwa kulifumbua fumbo hili, na badala yake kunasa kwenye mtego. Utasikia, kwa mfano, mtu anasema “Hitaji langu muhimu kwa sasa ni kazi!”
La mwisho, kwa leo ni hili la ukweli kwamba si kila jina lenye umbile la kiambishi ma- basi limo kwenye kundi hili la LI-YA. Majina kama mahakama na makala ni mfano wa majina yenye umbile hilo, lakini hayamo kwenye kundi la LI-YA
Yatoshe kwa sasa.
Kutoka kwa Khelef Nassor kupitia mtandao wa Facebook, tarehe 19 Januari 2011:
“Kiukweli uncle upo sahihi. Kwa upande wangu mm naomba niongezee hapo kwenye unasiabu wa lg, tunapozungumzia unasibu wa lg tunaangalia ktk sehemu kuu (3),kwanza ni kuwa mwanaadamu hazaliwi na lg isipokuwa huikuta ktk jamii hivyo basi kuikuta kwake huko ndio tunasema ameikuta kwa nasibu. Pili, ktk upangaji wa sauti na kuziweka ktk mfumo wa mawasiliano inategemea na wale wanaoanzisha lg, mfano,sauti /d/,/u/,/k/,/a/ambazo tunapata neno duka, wenye lg walikuwa wanauwezo wa kuzibadilisha sauti hizi na kupata neno (kadu) hivyo basi upangaji wa sauti hizo tunasema ni wa nasibu. Tatu tunasema kuwa hata sauti zinapokuwa zimepangwa kuwa maneno bc maneno hayo huwa niyanasibu kwani kunakuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno na kioyevu chenyewe,mfano,neno sukari kunakuwa hakuna uhusiano kati ya neno sukari na sujari yenyewe. (Ni hayo tu.)”