KISWAHILI KINA WENYEWE

Upekee wa Kiswahili: Uambishaji na Urejeshi

Ujuzi wangu kwa lugha nyengine zisizokuwa Kiswahili si mkubwa sana. Sisemi pia kuwa ni uweledi mkubwa wa lugha yangu ya Kiswahili. Lakini huo mdogo nilionao katika lugha za Kiingereza, Kijerumani na Kiarabu umenifanya niamini kuwa miongoni mwa tafauti na, hivyo kinachojenga upekee wa Kiswahili, ni dhana hizi mbili – uambishaji na urejeshi.

Na hapa ni bora nikakiri na mapema kwamba uelewa mdogo hautoshi kujenga hoja ya kitaaluma. Kwa hivyo, sitaki maandishi haya yachukuliwe kuwa hoja ya kitaalamu, bali zaidi mazungumzo ya mzawa wa lugha ya Kiswahili, mwenye kufahamu mawili matatu kuhusiana na lugha yake na ambaye angelipendelea kuchangiana maarifa hayo madogo na wengine. Lengo ni kuyakuza maarifa hayo madogo yawe makubwa na yatanuwe mawazo ya pande zote zitakazojihusisha na mazungumzo haya.

Uambishaji

Katika uzoefu wangu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa Kijerumani, hakuna wakati darasa linapochangamka kama wakati wa mada ya uambishaji, na mahsusi kwenye kitanzi. Kuambisha ni kuweka viambishi kwenye mzizi wa neno ili kutoa maana inayokusudiwa. Kiambishi huweza kubadilisha kitenzi kuwa nomino, nomino kuwa kivumishi, kitenzi kuwa kielezi na, juu ya yote, uambishaji kwenye Kiswahili hukifanya kitenzi kimoja kuwa sentensi nzima yenye sehemu zote kuu tatu – mtenda, kitendo, mtendwa, hali ya utendaji.

Ukiacha Kiarabu, ambayo nayo inaruhusu kiwango fulani cha uambishaji kwenye kitenzi, ni lugha ya Kiswahili ninayoiona inaongoza. Nakubali kusahihishwa ikiwa nimekosea. Hata hivyo, hebu angalia mfano huu na neno moja tu “Nimemuona” ambayo kama ingelitafsiriwa kwa Kiingereza au Kijerumani, yangelikuwa maneno manne:

Kiingereza: I have seen him/her.
Kijerumani: Ich habe ihn/sie gesehen

Ndani ya neno moja la Kiswahili, muna kila kitu kinacholifanya kuwa sentensi kamili:

Ni- inawakilisha kiambishi cha nafsi ya kwanza umoja – mimi, mtenda
-me- inawakilisha kiambishi cha hali timilifu ya wakati uliopita
-mu- inawakilisha kiambishi cha nafsi ya tatu umoja – yeye, mtendwa
-on- inawakilisha mzizi wa kitenzi – kuona
-a – inawakilisha kiambishi cha hali ya kitendo – utendaji

Sentensi nzima imesemwa kwa neno moja tu na maana kamili ikakamilika.

Urejeshi

Hoja hapa si kwamba Kiswahili pekee ndicho chenye urejeshi, lakini ni kwamba dhana hii ni pana sana kwenye lugha hii kuliko kwa lugha nyengine. Viambishi na vipashio vya Kiswahili vinavyotumiwa kuwakilisha urejeshi ni vingi na vinakutikana katika mazingira mbali mbali.

Suali la kwanza kulijibu ni maana ya urejeshi kama dhana kwenye muundo wa lugha. Dhana hii inawakilisha viambishi au vipashio vya maneno yanayorejelea nomino, viwakilishi au vivumishi kwenye maneno. Katika sentensi hii, kwa mfano, “Ni yeye mwenyewe ndiye mwenye matatizo, sio mimi,” maneno yaliyokozeshewa wino, yote ni virejeshi.

Kwa Kiingereza, sentensi hii ingelisomeka: “It is he/she himself/herself who has got problems, not me.” Pengine tafsiri hii si sahihi kuelezea dhana kamili kwa lugha ya Kiingereza. Na hapa ndipo ninapohoji upekee wa Kiswahili. Kwamba urejeshi wake ni mpana sana. Katika mfano huu, maneno mwenyewe, ndiye na mwenye yanarejea kwa kwa kiwakilishi yeye, ambacho nacho kinasimama kwa nafsi ya tatu umoja, inayoweza kuwa Asha au Juma.

Zingatia jambo moja muhimu sana hapa: kwamba maneno yote matatu yanazingatia kile kinachoitwa “upatanishi wa kisarufi”, yaani utawala wa nomino (kiwakilishi) kwa aina nyengine za maneno kwenye sentensi.

Dhana hii ya upatanishi wa kisarufi, ambayo kwa undani inafafanuliwa kwenye makala nyengine, inashurutisha kuwepo kwa uwiano kwa aina ya kundi la nomino na maneno mengine yanayohusu nomino hiyo, viwakilishi vyake, vivumishi vyake na hata vitenzi. Katika mfano wa hapo juu, maneno hayo yanawiana kama hivi:

  • Yeye = kiwakilishi nafsi ya tatu umoja kinachosimama kwa kundi la YU-A-WA. Anaweza kuwa mtu, mnyama au ndege. Katika mfano wetu, bila ya shaka amekusudiwa mtu, anayeweza kuwa mwanamke au mwanamme.
  • Mwenyewe = kipashio cha urejeshi kinachosimama kumaanisha “huyo hasa”
  • Ndiye = kipashio cha urejeshi kinachosimama kumaanisha  “ni yeye ambaye”
  • Mwenye = kipashio cha urejeshi kinachosimama kumaanisha “aliye na

Urejeshi katika Kiswahili haumalizikii kwenye hivi vinavyoweza, peke yake, kuitwa viwakilishi, bali umo pia ndani ya vitenzi kwa kupitia viambishi –ji- na pia –o- (mara nyengine –ye-).  Mifano hii inathibitisha hayo:

  • -ji-: Watoto wamejipaka rangi
  • -o-: Watoto waliojipaka rangi wamependeza
  • -ye-: Mtoto aliyejipaka rangi amependeza

Ambapo –ji- ndani ya kitenzi inarejea dhana ya ‘kujitenda’, -o- na –ye- zinarejea kwa mtendaji mwenyewe (kwa hapa) au katika mifano mengine mtendwa.

Huu ndio ninaouita upekee na upana wa dhana za uambishaji na urejeshi kwenye Kiswahili.

14 thoughts on “Upekee wa Kiswahili: Uambishaji na Urejeshi”

  1. Kirejeshi ni kipashio cha neno kinachorejelea ngeli au mtendaji.kuna aina mbili ya virejeshi :-o-rejeshi na -ji-. Kuna ana mbili ya -o-rejeshi,-o-rejeshi awali na tamati kulingana na ngeli husika. Mfano: aliyesoma na asomaye.kirejeshi -ji- hutumika kurejelea mtendaji.mfano amejikata.

  2. Asanteni sana kwa juhudi zenu za kukuza lugha hii ya kiswahili lakini nina swali lanitatiza sana hapa, utofauti uliopo kati ya uambishaji na unyambulishaji.

    1. Ahsante nawe Kaloz Gabriel kwa kutembelea mtandao huu na kwa swali lako. Uambishaji ni dhana inayowakilisha upachikaji wa vipashio vya kisarufi kwenye mzizi wa neno kwa minajili ya kujenga ama neno jipya au kubadilisha tu hali ya neno. Kuna viambishi awali, kati na tamati, kwa mujibu wa wapi kinakaa kwenye huo mzizi wa neno. Kwa mfano, mzizi wa neno -pig- ukiwekewa viambishi ku-pig-a unakuwa kitenzi au kitenzi nomino na ukiwekewa pig-o unakuwa nomino. Inaweza kuwa u-pig-aji, ma-pig-ano, m-pig-aji na kadhalika.

      Unyumbuaji kwa upande wake ni kuvichambua hivyo vipashio vilivyounganishwa kwenye neno moja na kuvipa tafsiri yake ya kisarufi. Kwa mfano, neno (au sentensi) “ninakuona” inaweza kunyumbuliwa hivi ifuatavyo:

      i. ni-: kiambishi awali cha nafsi ya kwanza umoja, yaani mimi, katika hali ya utendaji
      ii. -na-: kiambishi awali kinachowakilisha wakati uliopo
      iii. -ku-: kiambishi awali kinachowakisha nafsi ya pili, umoja, yaani wewe, katika hali ya utendwaji
      iv. -on-: mzizi wa neno wa kitenzi ona
      v. -a: kiambishi tamati kinachowakilisha hali ya utendaji

      Kwa hivyo, kwa muhtasari uambishaji ni upachikaji vipashio vya kisarufi kwenye mzizi wa neno na unyumbulishaji au unyumbuaji ni upachuwaji wa vipashio hivyo na kuvichambua maana yake kisarufi.

      Nataraji jibu hili limesaidia.

      1. Ndugu Ghassani, katika unyumbuaji umeniacha hoi. Tafadhali pitia vitabu tena

    2. uambishaji ni kitendo cha kupachika viambishi awali na tamati mbele na nyuma ya mzizi wa neno wakati unyambulishaji ni kitendo kupachika viambishi tamati tu mbele ya mzizi wa neno

  3. Urejeshi huweza kutokea katikati ya kitenzi Kikuu kmf. anayekuja ,mwishoni mwa kitenzi kama alalapo au kwenye mzizi wa AMBA kama ambaye

  4. mambo muhimu ya kuzingatia ili urejeshi uweze kutokea ni yapi?
    namna tatu za kuambika “kiambishi rejeshi” ni zipi?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.