KISWAHILI KINA WENYEWE

Ng’ang’ania

Rafiki yangu mmoja kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, Mvukuchani Alfaraghany, ameniomba nilifafanue neno ‘ng’ang’ania’, akiamini kwamba linaandikwa na pengine kutamkwa na kutumika sivyo. Ufuatao ni uelewa wangu kwa neno hilo katika viwango vya muundo na maana yake:

Muundo

‘Ng’ang’ania’ ni kitenzi katika jumla ya vitenzi vya Kiswahili vyenye mashina ya lugha za Kibantu. Ni miongoni mwa vitenzi vyenye silabi nyingi na zinazojirejea katika mzizi wake. Mifano mingine ya vitenzi kama hiki ni ‘tetea’, ‘chechea’ na ‘tutumua’, kwa kutaja michache. 

Jengine la muhimu zaidi katika muundo wa kitenzi hiki, ni kuwa kwake na sauti ya ‘ng’ ambayo pamoja na ‘ny’ zinawapa shida wageni wa lugha hii. Uzoefu wangu kwa wanafunzi wangu wa Kiswahili kutoka Ujerumani, ni kwamba huwachukuwa muda mrefu kumudu sauti hizi. Ajabu ni kuwa hata wazungumzaji wa Kiswahili wa muda mrefu, ambao Kiswahili si lugha yao ya kwanza, nao wanakabiliwa na ugumu huu. Badala ya ‘ng’ombe’, kwa mfano, hutamka ‘ngombe’.

Kitenzi ‘ng’ang’ania’ kinaweza kuambishwa kama kilivyo kitenzi chochote cha Kiswahili, na katika uambishaji huo hakipotezi mzizi wake. Kwa mfano, kinaweza kuwekwa viambishi awali na tamati na kuwa nomino kama vile ‘ung’ang’aniaji’, ‘ung’ang’anizi’ au ‘mng’ang’anizi’.

Ninachosisitiza hapa ni kwamba mzizi wa neno hili ni ‘ng’ang’ani-‘ na sio ‘ng’ang’an-‘, kama ambavyo kimakosa hutumiwa na watu siku hizi, hasa Tanganyika, ambako kumezuka neno ‘ng’ang’ana’ (wengine husema ng’ang’anaa) kwa maana ile ile itumikayo kwenye Kiswahili kwa neno halisi la ‘ng’ang’ania’.

Maana

Wakati naandika ufafanuzi huu, karibu yangu hapana kamusi lakini nimezaliwa na kukulia kwenye mazingira ya lugha ya Kiswahili, ambapo nimepokea maana ya ‘ng’ang’ania’ kuwa ni ‘shikilia kwa nguvu’ kama ilivyo kwenye mfano wa mtoto anapomng’ang’ania mama yake, aidha kwa khofu au kwa mapenzi.

Katika mifano mingine, unaweza kumsikia mmoja akimwambia mwenzake: “Ng’ang’ania hapo hapo, hata akikuuliza mara ngapi, usibadilishe jawabu.’ Maana yake ni kuwa shikilia kwa nguvu msimamo wako.

Kwa hivyo, neno hili huweza kutumika kumaanisha kushikilia kwa nguvu kitu halisi au dhana.

Ni hayo kwa sasa.

1 thought on “Ng’ang’ania”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.