Mtihani mmoja ninaokabiliana nao katika kufanya kazi ya uandishi wa habari kwenye chombo cha kimataifa, ni kutafsiri taarifa kutoka lugha za kigeni, kama Kiingereza na Kijerumani, kuja lugha ya Kiswahili. Na ni mtihani si kwa sababu ya uwezo mdogo kwa lugha hizo, bali kutokana na ukweli kuwa lugha ni kielelezo cha tamaduni na maana ambayo watu wa utamaduni fulani huyapa mambo na dhana katika maisha yao.
Matokeo yake ni kwamba ni.nadra sana kukuta pana tafsiri ya neno kwa neno kutoka lugha moja kwenda nyengine, hasa inapotokea kuwa lugha hizo zinawakilisha tamaduni zinazopishana sana kijiografia, kiimani na kiteknolojia. Mtu asipozingatia ukweli huu, ndipo anapoishia kulazimisha matumizi ya misamiati kuwasilisha dhana ambazo hazieleweki kwa walengwa. Kwa mfano, utasikia mtangazaji anasema: Rais wa Guinea alikufa pale ‘akipokea’ matibabu Ufaransa.
Hiyo ni tafsiri ya neno kwa neno
ya “the Guinean president died while receiving medical treatment in France.” Lakini mantiki ya lugha ya Kiswahili haikubali tafsiri hii. Kwa mfano inataka patumike tafsida ya ‘kufariki au kuaga dunia’ badala ya neno kavu ‘kufa’ na sio ‘pale akipokea’ bali wakati akipatiwa matibabu, maana kwa utamaduni wa Kiswahili matibabu hayapokewi ila hupatikana.