Mzigo umetushinda, na sasa tunautua
Achukue anopenda, bure tunamgaia
Naende nao pa kwenda, atie pa kuutia
Kila tulipouweka, tulihisi maumivu
Kichwa kilitonesheka, zikaumia na mbavu
Ni kwa nini kuteseka, tukazinga ulemavu?
Mzigo umetuchosha, kale tuliojitwisha
Leo hii twaushusha, mbele kutoufikisha
Chukuweni twanadisha, utakayemridhisha
Twatokanao baidi, mzigo huu mujue
Tukafanya ukaidi, tupoambwa tuutuwe
Ila sasa ishabidi, mzigo uwachiliwe
Ni bora nusu ya shari, kuliko shari kamili
Na ndipo tukakhiyari, zigo kulitupa mbali
Kila lililo hatari, kukwepa mustahili
Wala kushindwa si ila, zigo twalitupa kule
Kikushindacho kukila, asilani usikile
Ikikukumba thakala, hupaswi ambiwa pole!
Seif Njugu
4 Januari 2011
Zanzibar
Mzigo wa misumari, kichwa bure takuchoma
Kujitwisha sishauri, labda kuusukuma
tunauaga kwaheri, nauendevye daima