Nipokee mshairi, kwa moyo wa maridhia
Niji na langu shauri, moyoni nimelitoa
Mungu ’takulipa kheri, na ubora wa afia
Nimekiweka cha kwangu, nipate kukata kiu
Ninatokea safari, kusaka mafanikio
Sijatembea kwa gari, silo langu kusudio
’Taonekana jeuri, kukosa matarajio
Nimekiweka cha kwangu, nipate kukata kiu
Lengo langu ni kisima, kilicho cha peke yangu
Hata kama nusu pima, lakini kiwe cha kwangu
Sitaki jirani mwema, nikiteke peke yangu
Nimekiweka cha ndani, nipate kukata kiu
Tele huko majiani, visima na sivitaki
Hata kwa wangu jirani, na maji hayakauki
Kiu yangu kisirani, kamwe hainiondoki
Nimekiweka cha ndani, nipate kukata kiu
Hivyo vina kamba nyingi, kila mtu mchotaji
Huchotwa bila msingi, na wenye kiu ya maji
Hata akiwa kidingi, mradi awe mywaji
Nimekiweka cha ndani, nipate kukata kiu
Wataniita mchoyo, ila silo lengo langu
Kuchanganya na mwenzio, sitokyeta tena changu
Na kiu niliyonayo, haitotoka wenzangu
Nimekiweka cha ndani, nipate kukata kiu
Nisameheni wenzangu, chimbeni vil’o vya kwenu
Kisima cha peke yangu, sitochota vilo vyenu
Niikate kiu yangu, za kwenu shauri zenu
Nimekiweka cha ndani, nipate kukata kiu
Suleiman Mkubwa (Tajiri wa Ushauri)
27 Disemba 2011
Zanzibar