Fukara hathaminiki, wahenga walishasema
Na wala hatambuliki, itapokuja neema
Kutwa yupo kwenye dhiki, hajui yake khatima
Tatizo yeye fukara
Watapendana kwa dhati, moyoni watashibana
Watapanga mikakati, na ahadi kupeana
Wazazi hawalitaki, ugomvi watashindana
Fukara hathaminiki
Atajawa na busara, hekima tele kichwani
Kulitoa lilo jema, kueleza hadharani
Hata hawatolipima, ni kwa faida ya nani
Fukara hana sauti
Hata kama ni sheria, fukara ndo kosa lake
Watakaa kuamua, kumnyima haki yake
Hana pa kukimbilia, abaki ahangaike
Fukara hatambuliki
Na hata akiokota, fukara huwa kaiba
Ni wapi atapopata, njia zake ukiziba?
Kakosa pa kukamata, ufukara ni msiba
Fukara yupo tabuni
Hata akifanya nini, fukara yupo tabuni
Hajui leo ni lini, kutwa kucha mashakani
Hujui yu furahani, ama yupo msibani
Fukara hatambuliki
Suleiman Mkubwa (Tajiri wa Ushauri)
27 Disemba 2011
Zanzibar