Nelisomapo shairi, la nduu yangu
Mwingi wa umashuhuri, aso majungu
Kwa kina kitafakari, jawa utungu
Mwishowe alitongoa!
“Tamu hetuzidiriki, msemo wake
Hata ukipata dhiki, mfano wake
Utatenda yaso haki, yenye makeke
Kwavyo hetuidiriki”!
Kenitaka nimjibu, sababu zake
Kwa nini yanawasibu, wafedheheke
Wasotaka ya thawabu, na radhi zake
Na vino ninamjibu!
Ni ujinga lotusibu, tupumbazike
Na kuikosa aibu, usoni pake
Kila tunalojaribu, ovu tuweke
Kwa hivi twasulubika!
Ya dini yenye kusibu, thamani yake
Yenye heshima, aibu, na kheri zake
Sisi kwetu iwa tabu, tusiyashike
Kwavyo tunasulubika!
Mafunzo ya wetu babu, twapiga teke
Ya wazee maswahibu, tini tuweke
Twejiona ‘westarabu, tuelemike
Kumbe hadhi twejishusha!
Tamaa imetusibu, mbele tuweke
Uchoyo na usulubu, tujibweteke
Ulafi bila kutubu, na tuzeeke
Hizi ni mionogni mwazo!
Kukinai ya thawabu, kwa hili pweke
Sisi tweona ni tabu, tuadhibike
Na uchoyo aghalabu, rafiki yake
Kwavyo twashindwa diriki!
Narudi kwako sahibu, uelimike
Nadhani hustajabu, usiyumbike
Kwa uzuri wa majibu, yano niweke
Kwazo tusizodiriki!
Othman Ali Haji
24 Disemba 2011
Zanzibar