Kauli ‘liwashangaza, wakashangaa
Kameruni kutangaza, atakataa
Misaada ‘noagiza, kutuletea
Tanzania ikiwemo!
Kauli ‘lipotongoa, ‘kaianika,
Dunia ikasikia, ikagutuka
Madola ya Jumuia, ‘taadhibika
‘Kiukataa ushoga!
Mara wakajiinua, huku wang’aka
Viongozi ‘katongoa, ‘mekasirika
Wote wataoingia, ‘kajumuika
Ushogani ‘taumia!
Kwa ujuba na jeuri, wakatamka
Misada wahiyari, ikakatika
Na tena tuko tayari, njaa tukifa
Ela hatwebu ushoga!
Lakini ajabu yetu, inayotisha
Hivino vitendo vyetu, vyaogopesha
Viovu visivyo utu, unyama kwisha
Ila haya tweyajua?!
Siipingi Serikali, gamba kuvua
Kwa mdomowe mkali, kupapatua
Walakini ni muhali, kukubalia
Kwetu tukawaamini!
Umalaya hivi sasa, ‘meimarika
Ulevi ndio kabisa, ‘mezoeleka
Ulawiti watikisa, umetushika
Kipi mtatudanganya!?
Madanguro yamo mote, ‘mesajiliwa
Nanyi mwayajua yote, mwayatumia
La Kameruni ni tete, mwatuambia
Unafiki ni wa nini!?
Kama kweli mwayakana, ‘liyoeleza
Ya kwamba ni ya fitina, kuileteza
Mwashindwani hizi lana, kutokomeza?
Mwaja mukitudanganya!
Huo utayari wenu, u wapi sasa?
Hiyo mijineno yenu, umbo tasa
Sababu vitendo vyenu, vinawasusa
Ta’ lini ‘tatudanganya?
Othman Ali Haji
02 Disemba 2011
Zanzibar
Ewe Ochu sikiliza, nilinenalo
kula linopatiliza, likanye hilo
yule anotekeleza, msuse nalo
Mbawa zinyonyowe
Wahenga watueleza, bila utata
kuchukia ni kuanza, kupiga vita
msitu kuteketeza, chechea ndo stata
hata maji machafu yazima moto!
Uovu auonaye, auondoe
Mikono aitumiye, athari isibake
ulimi ashambuliye, au achukie
Elfu huanza na moja
Alofanya jitihada, ‘simdharau
hakuna kiso faida, japo kichunguu
piopio ndio ada, alovunjika mguu
alothubutu si kama alogugumia
Nesikiya unenayo, e kijana Ahmedi,
Wanona nekoseyayo, kutoutamba weledi,
Negeuka mpitayo, kela kitu nihasidi,
Na sasa wataka jibu!
Sikia nonena kwako, nakwamba uwe shahidi,
Nti hii walo wako, na wezazi wa shadidi,
Wevita wapiganako, mema kuzidi shadidi,
Na leo twayona yayo!
Maadili yaloyepo, na adili ilozidi,
Ushuwari wa upepo, rehema Mola ‘lozidi,
Yeharibiwa kwa upo, nao wetenda kusudi,
Sasa leo twewa wapi?
Si kama niliyakana, waloyao ya usudi,
Neyasifu niyaona, ni mema yenye kusudi,
Tena yafaa kuyona, kwetu yawe ni waridi,
Ela wakweli kivitendo?
Kama ni wakweli sasa, waanze kuyahusudi,
Mabaa, zinaa sasa, wazondoe kwa kusudi,
Ulawiti wanoasa, waadhibiwe khuludi,
Tena iwe kwa vitendo!
Maneno walotongoa, hayatafawa abadi,
Kama hawatajandaa, kuyondoa asilidi,
Tena wajona wafaa, vitendo wavihasidi,
Tuseme wekusudiya?
Othman Ali Haji.
03/01/2012,
Zanzibar.