Anita kishuna wangu, nende nikamliwaze
Anita yuna machungu, miye nikayapunguze
Anita kwa jina langu, nazihisi pumzize
Naja, sitabisha naja!
Anita hamkumbate, hamzonge mikononi
Anita sauti yote, kwa siyahi na huzuni
Anita akanipe vyote, vilivyomwe maungoni
Naja, sitasita naja!
Anita aja usiku, nnalala kitandani
Anita ana shauku, hawe pake ubavuni
Anita yu ma’shuku, tukatiane machoni
Naja, nakwitika naja!
Anita kashajipamba, aningojea kwa hamu
Anita yukijiramba, yuajuavyo utamu
Anita ajua kwamba, lengo lake litaqimu
Naja, Zenji wangu naja!
Hamad Hamad
2 Disemba 2011
Copenhagen