Mapenzi kitu azizi, katujalia Manani
Mapenzi yatoka enzi,si ya leo duniani
Mapenzi ni ya Mwenyezi, kashusha kwa insani
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Wakupenda nachagua, si kama kila mmoja
Napenda alotulia, nikiona ipo haja
Sipendi viruka njia, ninaogopa viroja
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Wasichana wapo wengi, wanaojipendekeza
Wengine ni mashangingi, nahofu kunipoteza
Nina mambo ya msingi, kwanza ninayachunguza
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Simapembe pendo langu, kila mmoja apate
Nibasmati ya tangu, hailiwi na watu wote
Huliwa na wenye fungu, sio wewe patasote
Siligawi kama njugu, pendo langu mawambia
Napenda wenye nidhamu, ‘lofunzwa akafunzika
Na walo wataalamu, kiwa ndani huna shaka
Kwani hao ni walimu, kwa mapenzi ni hakika
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Hupenda wanaotunza, mambo yao ya nyumbani
Marufuku kutangaza, yafanyikayo chumbani
Sio kuihanikiza, kwa shoga na majirani
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Yule atakayefika, kuwa mimi nimpende
Basi amebahatika, bahatiye ya mtende
Jangwani wanawirika, miti mingine isende
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Kipenda napenda kweli, wala sifanyi utani
Pendo langu ni asali, tamu isiyo kifani
Lakini ni mbakhili, siligawii njiani
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Wale wananyemelea, walipate langu penzi
Samahani nawambia, kwa sasa nina mpenzi
Huyo ndo anonilea, anienzi namuenzi
Siligawi kama njugu, pendo langu nawambia
Mzee Haji (Sir Haji)
24 Novemba 2011