Mtu ameulizia, maana ya KAMA NINI
Mimi kwanza namwambia, lugha sio yake fani
Mana angelitambua, maana ya kama nini
Kama nini maanaye mithiliye huioni
Ukisema yu aavyaa, yu avyaa kama nini
Maana anavyovaa, mfanowe huuoni
Toto anazitotoa, nyingi zisizo kifani
Kama nini maanaye, mithiliye huioni
Mfano watu wa Kae, kanikaza kama nini
Maana ampendae, mithiliye huioni
Anampenda tujuwe, mwenginewe hatamani
Kama nini maanaye, mithiliye huioni
Hapo mtaposikia, kuna kura ya maoni
Basi msijekosea, muwe wengi kama nini
Muwe wengi kama nini, yetu yaende usoni
Kama nini maanye, mithiliye huioni
Nadhani atatambua, maana ya kama nini
Tamati ninafikia, naondoka darasani
Somo nimempatia, mifano imesheheni
Kama nini maanaye, mithilite huioni
Hapa tena sitaraji, mbele mimi kusogea
Naondoka Sir Haji, kwengine naelekea
Kitu ninachotaraji, jawabu imetulia
Kama nini maanaye, mithiliye huioni
Mzee Haji (Sir Haji)
24 Novemba 2011