Wengi tunavitamani, vile vilo kiririni
Tuvitie mkononi, tuseme sasa shuwari
Lakini ni hamkani, tena kikiri kikiri
Hatupati kwa utashi
Kweli tunavyotamani, vingi tunastahiki
Lakini vimikononi, mwa wenye kutudhihaki
Wao huwa farahani, kihisi twapata dhiki
Hatupati kwa utashi
Mija na moja ni tatu, babu alituambia
Sijui hesabu zetu, wapi tunaelekea
Kama ni za babu zetu, au twageuza njia
Hatupati kwa utashi
Mjini na vijijini, mimi ninawashtua
Kwa haraka amkeni, tuanze kujitetea
Tusiwe vibarazani, uwanjani twakimbia
Hatupati kwa utashi
Bila matendo aushi, haja zetu hazijiri
Hatupati kwa utashi, hata vitu vya hiari
Hupata kwa ushawishi, bidii pia dhamiri
Hatupati kwa utashi
Sir Haji nishasema nadhani mumesikia
Kama ndio himahima, mbele tungesogelea
Waume na kinamama, hakuna wakubakia
Hatupati kwa utashi
Mzee Haji