UCHAMBUZI

‘Katiba Mpya‘ yaweza kuidhoofisha CUF kama ufisadi kwa CCM

Kutoka kushoto: bendera ya Zanzibar, ya CUF na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. CUF imewekwa kati?

Baada ya kufuatilia alichokisema leo (22.11.2011) Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakari, kuhusiana na kadhia ya mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na namna kilivyopokelewa na wachangiaji kadhaa kwenye majukwaa ya mtandaoni, utabiri wangu ni huu kwa Zanzibar: katika uchaguzi wa 2015, vyama vyote viwili vinavyounda leo Serikali ya Umoja wa Kitaifa vitakuja kulazimika kuiba kura kusalia madarakani.

Swali ni kuwa vitamuibia nani wakati vyenyewe ndivyo pekee vinavyozimiliki siasa za Zanzibar hadi sasa? Jibu ni kuwa, hadi jana ilikuwa kweli kuwa CCM na CUF pekee ndivyo vyama vilivyotawala siasa za Zanzibar. Lakini si leo tena. Leo kundi la tatu linaibuka, likiwa na kete ile ile ambayo iliipa uhalali CUF tangu kuanzishwa kwake – upinzani wake wa wazi dhidi ya mfumo wa Muungano.

Ninaweza kukosolewa kwa kuulizwa, kundi hilo nimeliona wapi, nami sipo Zanzibar hivi sasa. Na nikijibu mtandaoni, nitakosolewa tena, kwamba siasa za mtandaoni (desktop politics) sizo zinazoiendesha Zanzibar. Siasa za Zanzibar ziko chini kwenye umma, ambako hata hiyo fursa ya kutumia mtandao haipo kwa sehemu kubwa ya watu. Huko kwetu Shengejuu na Mangapwani hakuna watumiaji wa Facebook, Twitter, YouTube na MzalendoNet. Kwamba watumiaji wengi wa mtandao ni Wazanzibari wa tabaka la kati na, au, walio nje ya nchi, ambao hawafiki kwenye sanduku la kura.

Ila mimi, kwa ukaidi, ninashikilia kuwa kundi hili lipo na naweza kunusa athari yake. Kundi hili, ambalo hadi sasa si rasmi wala haliko chini ya chombo kimoja mahsusi, linaongozwa na mchanganyiko wa hoja za uzalendo na hamasa za ujana. Kuna uwezekano mkubwa kuwa, wengi wao ni wafuasi wa CUF, ambayo msimamo wake dhidi ya Muungano uliipatia uungwaji mkono mkubwa ndani na nje ya chama. Lakini kundi hili sasa linakwenda mbali zaidi ya pale CUF ilipowahi kufika, kwa kutaka na kutamka waziwazi kwamba Muungano uvunjike na Zanzibar iwe huru. Na haionekani kuwa kuna chengine chochote, pungufu ya hicho, kitakachokubalika kwao.

Hii ni lugha kali na ya mkato. Lakini ndiyo inayopendeza masikioni mwa Wazanzibari walio wengi, na bahati mbaya ni lugha isiyoweza kutamkwa rasmi na CUF wala CCM. Wengi wetu, ambao si wanasiasa, hatujui kunga za sanaa ya majadiliano – ya mpa-n‘kupe (give ‘n take), ambayo Waziri Abuu anasema ndiyo iliyoifanya serikali kushawishika na mswaada wa Uundwaji Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya. Hoja yake? Kwenye mambo 13 ya msingi yaliyotakiwa na Serikali ya Zanziba, 10 yameingizwa, matatu tu ndiyo yamewachwa. Kumi yepi? Matatu yepi? Ni maswali niliyoyakuta kwenye mitandao, na kwa kuwa hayakuwa na majibu, ndipo unapoona urahisi wa kutupata wengi wetu kwenye uungaji mkono wa kundi hili linaloibuka, kwa sababu linazungumza lugha yetu – lugha ya mkato, ya mfuto!

Kwa hivyo, kama ambavyo mada ya ufisadi imeijeruhi CCM kwa upande wa Tanganyika, ndivyo ambavyo ya Katiba Mpya itaijeruhi zaidi CUF iliyo kwenye serikali ya pamoja Zanzibar. CUF inajikuta majeruhi mkubwa kwa sababu niliyoitaja hapo juu – kwamba uhalali wake kwa Wazanzibari wengi ulikuwa ni msimamo wake kuelekea Muungano. Msimamo huu uliifanya kuungwa mkono hata na wanachama wa CCM.

Natamani kusema kuwa bado msimamo huu unaifanya CUF kuungwa mkono na hao wanaoiunga mkono, nikiamini kuwa haujabadilika. Lakini wakati umeshabadilika; na sasa msimamo wake wa mwanzo hautoshi tena kukidhi matakwa ya sasa ya umma (au angalau kundi hilo ninalolitaja hapa).

Kutoka sasa hadi uchaguzi wa 2015, kundi hili la tatu linaweza kujikusanya na kuwa vuguvugu la kweli na rasmi la kisiasa. Wala sisemi kuwa nguvu hii ya tatu itakuwa na nguvu za kweli za kuchukuwa madaraka. Sisemi kuwa itakuwa na uwezo wa kuiondoa Zanzibar kwenye Muungano. Sisemi kwamba itakuwa suluhisho. Lakini nasema ipo na iko nje na juu ya hata vyama vya siasa vilivyopo Zanzibar.

Narudia. Athari ya nguvu ya kundi hili kisiasa, kwa vyovyote vile, itakuwa ni kwa CUF. Maana CUF ndiyo imekuwa alama ya ‘ukombozi‘ wa Zanzibar. Kwa hivyo, ni CUF ndiyo inayopaswa kuishughulikia nguvu hii. Tena kwa kuifanya kuwa sehemu yake, na sio kuikandamiza.

Si lazima kwa CUF kujiondowa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kulifanya kundi hili kuwa sehemu yake. Lakini ni lazima ijiondowe kwenye kufungwa mikono nyuma linapokuja suala la Muungano. Kwa kiwango nilichomuelewa leo, Waziri Abuu ananifanya niamini moja kati ya mawili: aidha CUF, ambayo yeye anaiwakilisha serikalini, imefungwa mikono nyuma, au yeye hawakilishi msimamo wa CUF.

Sitaki kuamini kuwa wabunge wa CUF walipewa muongozo na chama chao kule Dodoma kushirikiana na CCM kuupitisha Muswaada wiki iliyopita, lakini yumkini Waziri Abuu aliwashawishi kwamba ni sawa kuupitisha kwa kuwa “maslahi yote ya Zanzibar yamezingatiwa kwa kiasi kikubwa“, kama ilivyokuwa kauli yake ya leo.
Hata hivyo, nataka kuamini kuwa kuna kitu fulani, mahala fulani, hakiko sawa. Kitu hicho kinalazimika kurekebishwa, sio tu kwa kuiepusha CUF na ‘ulazima‘ wa nayo kuiba kura mwaka 2015, bali kuiepusha Zanzibar kupoteza dira na muelekeo wake.

5 thoughts on “‘Katiba Mpya‘ yaweza kuidhoofisha CUF kama ufisadi kwa CCM”

 1. Sheikh Mohamed Khelef AL-GHASANY, Nimekuelewa vyema, na sasa nna uhakika, kwamba msimamo wako unafanana na msimamo wangu, msimamo wa khaleed Gwiji, msimamo wa Ally Saleh na wengine wengi. Hata Mheshimiwa Jusa Ladhu kwa maoni yangu ana msimamo kama wangu na wako, hivi ndo nnavyoamini mimi. Pia sikuona haja ya Mh. Abuu Bakari kuwalaumu kina Ally Saleh na wenzake, kama walifanya makosa basi makosa hayo yamesababisha na ukimya wao viongozi kutowajuulisha wananchi juu ya hatuwa waliofikia.Itakuwa jambo la ajabu kubwa kwamba mtu kama Ally Saleh ambae ameipigania Zanzibar kwa nguvu zake zote kuja kulaumiwa wzi wazi ati kwa sababu tu ameonesha shaka juu ya mwenendo mzima wa Mswada wa Kuanzisha Tume ya Kuratibu maoni ya wananchi kusuhu kuanzisha ka Katiba ya Muungano.

  Kwa ufupi wapo vijana wa Kizanzibari ambao wamewahi kuandika dissertations, thesis na nyaraka muhimu kuhusu Muungano. Baadhi ya vijana hawa ni Salmin Amour, ambae kwa hivi sasa ni naibu katibu mkuu Baraza la Mapinduzi, yeye katika dissertation yake ya Masters (LLM). Alitizama mamlaka ya Bunge la Muungano katika kupitisha Sheria zisizo za Muungano. Mh. Jusa Ladhu ameandika kuhusu Muungano katika dissertation yake ya LLB. Mohamed, ambae kwa sasa ni mwanasheria katika ofisi ya DPP nae ameandika kuhusu Muungano katika dissertation yake ya LLB. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud nae ameandika nyaraka mbali za kuvutia kuhusu maswala ya Muungano. Na hata naibu wa waziri wa Afrika Mashariki Mh. Mahadhi nae ameandika Kuhusu haki ya ZANZIBAR kujitenga katika Muungano kwenye mtazamo wa sheria za kimataifa.

  Wengine walioandikia kuhusu Muungano ni Mimi, ambapo Katika dissertation yangu ya M.A niliangalia sababu zilizopelekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuweza kuishi kwa zaidi ya miongo minne mbali ya matatizo mengi ambayo yanahatarisha uhai wa Muungano huu ( Why has the Union between Tanganyika and Zanzibar survives for more than four decades amid the challenges that threaten its sustainability). Sababu mbili kuu kwa ufupi ambazo niliziona ni utashi wa viongozi walioko madarakani (leaders’ interests) na Uwepo wa sheria zinazoulinda Muungano kwa nguvu zote ( Legal regime). Mfano mdogo wa sheria zinazoulinda Muungano, ni Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 ambayo pamoja na mambo mengine, inavitaka vyama vya siasa kuhubiri kuulinda na kuuimarisha Muungano. Kwenda kinyume cha matakwa ya sheria hiyo kunapelekea chama cha siasa kunyimwa ama kufutiwa usajili.

  Kwa maoni yangu, itakuwa si sahihi kufikiria kwamba CUF ambayo ni chama cha siasa kilichosajiliwa chini ya sheria ya vyama vya sisa ya mwaka 1992 kuweza kupinga Muungano wazi wazi. Mbali ya hoja hii, ikumbukwe kwamba CUF kwa sasa ni chama mwenza kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ZANZIBAR, serikali ambayo inaongozwa na Sera za CCM. Nionavyo mimi hili pia linachangia kupunguza hamasa za viongozi wa CUF walio ndani yaserikali kuweza kuupinga wazi wazi Muungano.

  Mbali ya hoja za hapo juu, kwa waliosoma siasa nadhani watakubaliana na falsafa ya Mtaalam Mmoja wa kifaransa ambayo inasema ” l’homme elu est l’homme perdu” kwa Kiingereza inasomeka kuwa “An elected man is a lost man”. Mimi nakubali kwamba kuwemo kwa viongozi wa CUF ndani ya Serikali ya umoja wa kitaifa kunadhoofisha nguvu zao za kuweza kuyapinga waziwazi mambo ambayo hawakubaliani nayo, hasa mambo yanayohusiana na Muungano. Pia ifahamike wazi kwamba viongozi waliochaguliwa kushika nafasi na uwaziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa wanawajibika kuonesha utii wao kwa Rais wa serikali waliyomo na sio misimamo ya vyama vyao, kwa mujibu wa falsafa ya mtaalam huyo wa kifaransa.

  Kuthibitisha hoja yangu hii, katika vikao vya Baraza la wawakilishi imeonekana wazi kwamba kumekuwa na tafauti kubwa ya kimtazamo baina front benchers na back benchers bila ya kujali misimamo ya kichama, kwa mfano, waheshimiwa Jusa ladhu, na Hamza Hassan walionekana kuwa mstari wa mbele kupinga hoja zilizotolewa na mawaziri katika baraza la wawakilishi, bila ya kujali waziri husika anatoka chama kipi cha siasa.

  Nini cha kufanya ? Kwa vile viongozi wa siasa kutoka vyama vya CUF na CCM wanaonekana kuwa na misimamo inayofanana linapokuja swala la Muungano, kitendo ambacho kiko tafauti na viongozi wa CUF na hata baadhi ya viongozi wa CCM ambao hawako katika Serikali kutokana na sababu nilizozieleza hapo juu, ipo haja ya sisi wenye mtazamo tafauti kuwahamasisha wananchi, na kuwaeleza nini cha kufanya itakapokuja kura ya maoni. Kwa maoni yangu ndio jambo pekee linaloweza kuikombowa Zanzibar.

 2. Ahsante sana Mohd Juma Abdalla kwa uchambuzi wako wa kina, wenye hoja na mifano. Naamini tunaweza kufika mahala tukayatengeneza haya tunayoona kuwa sasa yanaharibika. Zanzibar inatuhitaji sote, kila mmoja na mchango wake kuchangia ukombozi wake.

 3. salaam,

  nataka kusema kitu kimoja tu.

  hakuna mambo 13 wala nini. yangeweza kuwa 13 au 3.

  baada ya semina, samuel sitta aliyekuja kwa niaba ya kamati ya bunge ya katiba, alifanya sum up. na kwa fikra zake ni kuwa wawakilishi wali raise mambo 13.

  kwa maana nyengine ungekuwa wewe pengine ungeona 10, mimi 20 na kadhalika. inaonyesha abubakar khamis na wenziwe wameridhika na summing ya sitta na ndio maana wameshikilia mambo 13.

  pili, the point is abubakar khamis amepotoka kisheria kulaumu watu ku discuss bill iliyotolewa novemba 14 kwa sababu kisheria mpaka tunazungumza ile ndio bill halali.

  hata hivi leo hakuna mwenye bill mpya. baya zaidi hatujui kuwa waandishi wa bill hiyo mpya wata include nini na nini kilichokubaliwa kwa sababu utundu wa kuacha mambo umeshawahi kufanywa.

  chengine ambacho abubakar khamis ameki miss ni kuwa thrust of the mdahalo ilikuwa kuonyesha jinsi ambavyo serikali haikutimiza wajibu wake kama serikali kushirikisha umma katika mswaada huo mzito.

  na mimi nilisema moja ya premises mbovu ni kuwa wanasiasa kusema mswada huo ni wa kawaida kama miswada mengine, which is not true.

  nikuchekesheni kidogo: abubakar khamis anasema serikali ilishindwa kuwakusanya wananchi kwa sababu ya sikuu ya eid el haj? loo…hapo kanimaliza.

  nchi inaogopa siku kuu? mbona ziara zao toka imekwisha siku kuu zimeendelea? walokwenda UAE, waliokwenda dodoma, waliokwenda pemba…vikao vyao mbali mbali vimefanyika…na posho wameingiziwa….

  huu ndio uongozi tulionao sasa

  ally saleh

 4. Kwa kila hali, Abubakar ametuacha na maswali zaidi kuliko majibu aliyodhani ameyatoa. Ametuacha tukiwa hatumuamini zaidi kuliko alivyodhani kuwa ameziondosha shaka zetu kwake na kwa serikali. Kwa hili, tumenusa kufeli kwake, kwa serikali yake, na baya zaidi sasa wanataka kuifelisha Zanzibar kama walivyofanya watangulizi wao. Na adhabu ile ile ya kuwadharau waliopita kwa waliyotufanyia, sasa inaonekana kuwaelekea hawa waliopo sasa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.