‘Lidhani ‘tajikalia, kisubiri yako huba, kwayo uliyonitenda!
‘Takaa nikinyamaa, ‘kingoja yako suhuba, na mwili wangu ‘kikonda!
Chakula ‘tajimia, mai katu setashiba, kikufikiri kipendwa!
Kamwe siwi hayawani, enenda sirudi tena!!!
Enenda huko ‘tomea, kamwe kwangu nakwambia, “enenda katu serudi”!
Enenda nakuapia, sitawa mwana mkiwa, kwamba sina mburudi,
Tena nakuhakishia, nafasiyo ijaziwa, neshalipata waridi,
Enenda sejirudishe, sina haja nawe kamwe!
Enenda sijerudia, sifikiri tajiua, kukosa wako usudi,
Kama ulifikiria, kienda wewe tajuya, na kujiua tasudi,
Ukidhani haramia, takiteka kwa ubuya, na sasa tajihusudi,
Ulijidanganya sana!
Nakwamba nekuhakiya, fahamu sijeumiya, kwangu tena ‘serudi,
Sina pa kukuekeya, na moyo wangu hemiya, tena nazidi shadidi,
Ubakile hedithiya, athari kwangu sekoya, na kamwe haitarudi,
Enenda sirudi tena!
Othman Ali Haji,
20/11/2011,
Zanzibar.