Chini ya mkondo huu, nipo bado nateseka
Wao wameshasahau, huku walikoniweka
Kwa uzembe na dharau, ndipo haya yakatuka
Takwenda mwambia Mungu, sekufa niliuliwa
Ndivyo nitakavyosema, sekufa niliuliwa
Walijuwa lenda zama, kwani hawelizuwia?
Kama wejua si zima, kwani likaruhusiwa?
Sekufa niliuliwa, ndivyo Mungu tamwambia
Hii si mara ya kwanza, kwa Mungu tenda shitaki
Hii ni kuendeleza, walianza kwa bunduki
Ela hawenimaliza, wakaona haitoshi
Mungu takwenda mwambia, sekufa waliniuwa
Tasema yote hiwahi, kwa Mola wetu muweza
Tayasema ya Fatihi, walivyoniangamiza
Mbele ya zao nyajihi, nikafa wakinichunza
Sijafapo tenda sema, daima nehiuliwa
Sekufa waliniuwa, kwa kutaka na kusudi
Kisha wakatangazia, ‘kasema ndio ahadi
Hakuna alofidiwa, si ubani si kwa udi
Mungu takwenda mwambia, sekufa wanniua
Kifo changu kilijiri, kuwa kwao ni dhihaka
Wakaonesha viburi, hawetaka wajibika
Wakafichiana siri, hakuna aliyen’goka
Mungu yote wayajua, lakini taja yasema
Walipokwisha niua, changi wakazidiriki
Ati kuwasaidia, wale waliowabaki
Kwani hawewapatia, meli ilo madhubuti?
Ela hilo halitawa, waketaka nighariki
Ati waliunda timu, ya ajali kuchunguza
Wale wote mahkumu, ndio wakaiongoza
Vipi wangejihukumu, adala kuifanyiza?
Mola mie neuliwa, sekufa wanniua
Nipo chini ya bahari, nasubiri malaika
Wao watanisitiri, kama nyie hamwetaka
Ni sitara ya Qahari, sitara iso chafuka
Tubuni nawashauri, kabla siku kufika
Siku ya kwenda ungama, nenda simama hifika
Hawataje kwa majina, nyote muliohusika
Mulonacha hasakama, huku kusiko kalika
Rabi mjao sekufa, madhulumu neuliwa.
Hamad Hamad
September 25, 2011
Copenhagen