Si mboga kwa uhakika, nawaaseni wenzangu
Si mboga bali mashaka, hazina ila uchungu
Sifaye kuu kunuka, sizitake mlimwengu
Mboga zimea jaani, si mboga za kujiliya
Ukiziona sokoni, sha’ti zitakuvutia
Zimepangwa mafunguni, wengi wazikumbatia
Hazitowi vitamin, mwishowe watajutia
Si mboga za kujiliya, mboga zimea jaani
Kwa yakini mboga hizi, zinadanganya machoni
Si tungule za mchuzi, hata pya mabilingani
Sizile ndugu mayizi, usingie matatani
Mboga ziota jaani, si mboga za kujiliya
Mchicha sijeuona, kichani umetulia
Swahiba ukakazana, vicha kujinunulia
Utamu hutouona, machungu taambulia
Si mboga za kujiliya, mboga ziota jaani
Ukiwa huyaamini, maneno niyanenayo
Ukajitia kundini, kuiridhisha rohoyo
‘kazikomba za jaani, tajutia maishayo
Si mboga katu si mboga, mboga kutoka jaani
Said Yunus,
09 Julai 2011,
Selangor, Darul- Ehsan,
Malaysia.