Nataka nende nyumbani, haone wangu wavyele
Haanze walo Ziwani, Shengejuu hadi Ole
Hashibishe zao mboni, nami moyo utulile
Mola wangu niauni, lengo langu nifikile
Nataka nende nyumbani, hajikumbushe ya kale
Hakae msikitini, niwepo safu ya mbele
Hitakiwa niadhini, haraka bila sumile
Nende na maulidini, hale haluwa mabale
Nataka nende nyumbani, niliyako hasikizwa
Ngolengole midomoni, hichagiza hachombezwa
Hakorogewa ngaani, hap’wa sheli lya kupwazwa
Habwagwa vyangu chagoni, taratibu kwa kulazwa
Nataka nende nyumbani, hagowezane na watu
Gowe si la miilini, kuwana gowe papatu
Shitizai na matani, ndio silika ya kwetu
Hisha nirudi nyumbani, halumbe na wanakwetu
Nataka nende nyumbani, haonane na’lo wangu
Wangu kwa nje na ndani, wangu wa tangu na tangu
Wangu wa usingizini, wangu wa tamu na chungu
Lini tafika nyumbani, hatimize ndoto yangu?
Hamad Hamad
15 Juni 2011
Copenhagen
Kwa kwel hongera sana sana bwana Hamad, naam ahsante
Kun,chomoka mmalenga kumbe ndionkimya chote kile.. kilikua na mshindo mkuu.. hongera mashairi mazuri usisahau kutuletea hayo masheli yakupwaza. tu.