KISWAHILI KINA WENYEWE

Utamu Wake Shairi (Suali)

Nataka uliza swali, kuwauliza malenga
Wa karibu na wa mbali, wakomavu na wachanga
Musemao Kiswahili, kiarabu na kimanga
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Ni kupanga mistari, kwa vina ikapangika?
Iwe miwili miwili, mitatu na kadhalika
Maelezo amba swali, au jina kutajika?
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Ni taswira kusawiri, halisi ikaoneka?
Ukayachora mandhari, yanoweza kubalika
Ukaacha wafasiri, waseme wanavotaka?
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Ni mtiririko wake, wa fani na maudhui?
Vinofanya tusimkwe, tukawa hatujijui?
Tukataka tuyandike, ya rafiki na adui?
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Ni kuumba falsafa, nayo ukaiamini?
Ikawa si ya sadafa, bali imwako moyoni?
Imara bila khaifa, ukaweza kuihami?
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Ni ustadi muruwa, wa kuichezea lugha?
Kuinyambuwa nyambuwa, sarufiye na balagha?
Kwa ruhusa ulopewa, na leseni ya kilugha?
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Nipani jibu nipani, nipate nielimike
Mukishindwa niauni, nyamazani ‘sinicheke
Tamuuliza Ghassani, alonamba niandike
Ipi tamu ya shairi, tungoni inovutiya?

Hamad Hamad
08 Juni 2011
Copenhagen

1 thought on “Utamu Wake Shairi (Suali)”

  1. UTAMU WAKE SHAIRI.

    Kwa jinalo Rahmani, Mola wetu Msifika,
    Naomba uniauni, kwa hili ninalotaka,
    Naingia utungoni, mchango wangu kuweka,
    Unipe njema lisani, mazuri kuyatamka.

    Utamu wake shairi, Si betize kupangika,
    Si vina na misitari, kama inavyodhanika,
    Wala si kwa umahiri, wa maneno kurapuka,
    Tamuye ni kudhukuri, maneno yenye mipaka.

    Si tu mtiririko wake, wa fani na maudhui,
    Vifanyavyo tusimkwe, tuwe hatujitambui,
    Na vicheko tuvicheke, tuloambwa hatujui,
    Hiyo siyo tamu yake, tungoni inovutiya!

    Utamuwe si wa fumbo, kwa watu kuwafumbika,
    Wala utata wa tungo, usoweza eleweka,
    Ya kweli na ya uongo, tungoni ukayaweka,
    Si tamuye asilani, tungoni inovutia.

    Hasa ladhaye shairi, ni tungo za umakini,
    Si tungo za ki urari, wa vina wala mizani,
    Ni tungo zilo sheheni, mazuri yaliyo ndani,
    Na iwe mantikiye, kuadilisha jamia.

    Ladhaye siyo ya nyimbo, ya sauti kuighani,
    Kuitilia mapambo, na sherehe uwanjani,
    Lazima uwe na jambo, la kuweka hadhirani,
    Ili wajifunze kwalo, watakaolisikia.

    Ladhaye huzidi tamu, maneno yakipangika,
    Yenye kutoa elimu, watu wakaadilika,
    Ujumbewe ukadumu, muongozo ukatupa,
    Ndiyo tamu ya shairi, tungoni inovutiya.

    Sina mengi ya kunena, nisije nikakuchusha,
    Uwanda bado mpana, wapo watokujibisha,
    Kwa marefu na mapana, na maneno ya kutosha,
    Hoja utaianzisha, kama hukutoshezeka.

    BY: Amour Elfarssy.
    Mzanzibaria Halisi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.