Nazingwa ni ndugu zangu, wasonijua nilipo
Waumia kwa uchungu, kila wanikumbukapo
Waniombea kwa Mungu, mafanikio na pepo
Numonumo ndilo langu, tenda, tarudia kuko.
Nazingwa ni mafatani, wanitakao ninene
Wanichokoza kwa shani, wataka tutukanane
Muungwana situkani, kajaribuni kwengine
Sebu zingwa niachani, zingani kazi mufanye
Nazingwa kwa kila hali, nazuiliwa ‘sione
Naekewa majivuli, ya watu walo wanene
Dhamiri yao ya kweli, choneshwacho nisichone
‘sinizinge tafadhali , nachani nami nione
Nazingwa sikudunguwe, zikakufanyiza choyo
Si zako zina wenyewe, mja sema na rohoyo
Ngoja nazi zifuliwe, wombe nga’ ya kijiyo
Sipopewa sichukuwe, jilindiye hishimayo
Hamad Hamad
24 Mei 2011
Copenhagen