Wanitaka niwe wako, ati wa ubani
Niwe wako mali yako, niwewo mwandani
Siliwezi penzi lako, sebu abadani
Bora kaa peke yako, uwe mbali nami
Ng’ande huna cha kunipa, nikapendezewa
Nakwona watapatapa, wataka ghumiwa
Utakwisha hangaika, hutafanikiwa
Bora kaa pumzika, ‘sijedhihakiwa
Koya huna hata pendo, la kujikusuru
Kunahanikiza vundo, lanuka kufuru
Najibaidisha kando, usijenidhuru
Yamle na ya kidundo, najiweka huru
’Tasemaje wanipenda, na hunipi haki
Hata haki hiiwinda, wajipa hamaki
Kushanigeuza kinda, kesho haifiki
Nenda mwana wa kwenenda, sebu urafiki
Hamad Hamad
19 Mei 2011
Copenhagen