Dhoruba hii hakika, huchukua na kuzoa
Kwa wenye kubahatika, na kwa kipaji Jalia
Seuze wa tikatika, na wale mazoa zoa
Nani atabakia?
Imekuwa patashika, angani na bara pia
Watu wanahangaika, wapi watakimbilia
Kila mtu anataka, njia kujisafishia
Nani atabakia?
Usiku wahangaika, mchana wauchelea
Mbu huwa kwao shaka, hawajali malaria
Kusudi kunusurika, na janga la zahania
Nani atabakia?
Wapo wanomithilika, majabari wa dunia
Walizani wamefika, safari waloanzia
Hafla inatikisika, gari walioingia
Nani atabakia?
Tarehe ikitajika, huzunini huingia
Wanazidi taabika, shuwari inapotea
Kwa kweli wamahanika, na janga la zahania
Nani atabakia?
Najua mwapapatika, jawabu kunipatia
Katu si yangu dhihaka, kuona nasimbulia
Kwani ninachokitaka, najua mushatambua
Nani atabakia?
Amaan, Masoud Bakar
17 Mei 2011
Zanzibar