Uliniahidi, kwamba wenipenda ‘tanitumikia
Ukaitakidi, kuwa ‘tanilinda na kunitetea
Iwapi ahadi, mbona kushapinda wanigeukia?
Uliniapia, kwa Muumba wako hakuaminia
Nkasherekea, mikononi mwako mie kunitia
Sikufikiria, kwa tamko lako haya ‘ngenambia
Wejikubalisha, kwa khiyari yako ukanichukua
Sekukalifisha, ni utashi wako us’o na kinaa
Leo wanirusha, si changu ni chako kila ulotwaa?
Uliniambia, kila nitakacho utanipatia
Nkakutajia, ni hichi na hicho nakihitajia
Kumbe hwesikia, kunkuwa kocho wanimon’gonyoa?
Nekukaribisha, himayani mwangu mie hajiviza
Hakutawalisha, kila kilo changu uweze kitunza
Kushakinadisha, na kibanda changu wataka kiuza?
Sistahamili, kwa salata yako macho hafumbia
Napanga kitali, nikufate kuko nije kudungua
’Choka ufidhuli, na kiburi chako unonifanyia
Hamad Hamad
15 Mei 2011
Copenhagen