Haiwi!
Na wala haitokuwa
Kata’ani nakataa
Kuonewa!
Kubugudhiwa!
Kusulubiwa!
Kamwe haitokuwa
Kama ilikuwa
Basi ndio ilikuwa
Lakini katu haitokuwa
Kutuchezea
mulivyotuchezea!
Kutumezea
mulivyotumezea!
Kama ni kucheza
Tutacheza pamoja
Kama ni kumeza
Tutabwiya pamoja
Lakini kata’ani haitokuwa
Ilikuwa, ndio ilikuwa
Wakati huo
Mkajifanyia
Mlotaka kutufanyia
Mkatusomea
Mlotaka kutusomea
Mkatusemea
Mlotaka kutusemea
Lakini sasa Kata’ani
Kata’ani kufanyiwa
Kama nikufanya
Wenyewe twaweza fanya
Kama ni kusoma
Wenyewe tumeelimishana.
Kama nikusema
Tunavyo vinywa vipana.
Tutasema,
Tutatenda,
Tutafanya
Kwa nguvu zake Maulana.
Sasa tumeungama
Makosa tuliyoyafanya
‘Sirudi tena kiyama
hata kwa ipi namna
lazima kuyaondowa.
Haiwi!
Na wala haitokuwa
Kata’ani twakataa.
Kudhulumiwa!
Kukamuliwa!
Kudharauliwa!
Kamwe haitokuwa.
Kama ilikuwa
Basi ndio ilikuwa
Lakini abadani haitokuwa.
Kuharibiwa kiambo chetu!
Kuondolewa utu wetu!
Kufisidiwa jamii yetu!
Na kwanini ‘asa iwe kwetu tu?
Au mwatuona hatujui kitu?
Basi tambueni kama nasi’ ni watu
Tukisema basi hapa’wi n’tu
Ata pakiwa na mitutu
Lakini kata’ani tutapinga tu.
Ilikuwa, ndio ilikuwa
Zama hizoo
Mulipotupa nyama za ulimi
Nasi’ tukazifakamia
Mulipotupanda vichwani
Nasi tukawaridhia
Mlipofanya madhambi
Nasi’ tukawafagilia.
Lakini sasa kata’ani
Kata’ani kila neno kuaminia
Kwa sababu si mitume wala miungu wa dunia
Kata’ani kila jambo kuridhia
Kwa sababu si kila jambo hutiiwa
Kata’ani kila mfanyalo kusifia
Kwa sababu hata mitume hukosolewa
Seuze nyinyi msiofahamikiwa.
Tutachukia,
Tutapinga,
Tutaondoa
Rabi akitujaalia.
Sasa tumekarambuka
Utomvu umetutoka
Uhuru tunachotaka
Wakuyaondoa mashaka
Daima mtatukumbuka.
Said Yunus, Wete-Pemba, 2005