Raha ya maisha ni kutaka jambo katu ‘silipate
Ukalitafuta kwa vyote vsihindo usilifumbate
Hila zikakwisha ‘kabaki uvundo na misurumbwete
Na ndio maisha
Maisha rahaye n lyako kupata ukapigwa pute
Asiye mwenyewe akaja kupoka akamba n lyake
Mijitu ja mwewe ishalyaanika kwa laana zote
Na ndio maisha
Maisha yalivyo ni vile kutaka usichokipata
Kinyume ya hivyo wengine hupata wasichokitaka
Vivyo ndi viwavyo sote hatupata tungawa twataka
Na ndio maisha
Maisha mazuri mmoja ‘kipanda mwengine ashuka
Ni kama ratili juu haiganda chini haishuka
Hayamsitari uliotupanga sote ‘kanyooka
Na ndio maisha
Hamad Hamad
14 Mei 2011
Copenhagen