UCHAMBUZI

Utambulisho wa Zanzibar: Tulipojikwaa na tunapoweza kuinukia

Hapana shaka, inauma mno kukiri kwamba Uzanzibari unapotea. Na hata tunapofikia pahala pa kukiri hivyo, bado inatuwia vigumu kukubali kwamba unapotea kwa kasi ambayo ina maana mbaya sana kwa Wazanzibari wenyewe. Hatutaki kuamini kuwa tunapokuwa tumeshapoteza kila kile kinachosema kuhusu sisi, basi huwa tumeshapotea sisi wenyewe kama jamii ya kibinaadamu, maana huwa tumeshapoteza utambulisho wetu!

Na tunapopoteza utambulisho wetu kama jamii, tutawaacha wengine watutambuwe na watutambulishe sisi kwa jinsi wanavyoona wao inafaa. Watatuita wanakavyopenda na kutunasibisha na wanakachotaka kwa maslahi yao, bila ya kujiona na kosa, kwa kuwa wanavyojuwa sisi ni watu tusio utambulisho.

Narudia. Huu ni ukweli mgumu kuufahamu na mchungu zaidi kuumeza. Lakini ndivyo ulivyo. Akizungumzia ubaya wa kuwaachia wengine kukuumbia utambulisho wako, Malcolm X alisema hivi:

Mbinu mbovu na mbaya zaidi ya zote (inayotumiwa na Wazungu) ni kututambulisha na kutuita sisi (Wamarekani wenye asili ya Afrika) Waniga. Tunapokubali jina hilo na kujinasibishia, basi huwa tumejinasisha wenyewe katika mbinu yao hii…… lakini ukweli ni kwamba sisi sio Waniga na kamwe hatukupata kuwa Waniga, hadi pale walipotuchukuwa (kwetu Afrika) na kutuleta hapa (Amerika) na kutufanya tuwe hivyo.

Uniga umebuniwa tu na kutengenezwa kisayansi tu Wazungu. Ukimuona mtu anajiita menyewe Mniga, juwa huyo ni zao la ustaarabu wa Kimagharibi; na sio ustaarabu tu, bali pia uhalifu wa Kimagharibi….. Maana moja ya malengo makuu ya kuitwa kwetu Waniga ni kwamba tusijijuwe sisi tu nani hasa. Na ukikubali kujiita Mniga, unakubali kuwa hujijuwi, huijuwi thamani yako, hukijuwi kilicho chako wala hupajuwi palipo penu. Madhali wewe ni Mniga, basi huna hata kimoja cha kukiita chako.
(Malcolm X On Afro-American History, Pathfinder Press, uk. 15. Tafsiri ni yangu).

Huo ndio ubaya wa kumuachia mtu mwengine kukuumbia utambulisho wako. Unakugeuza dhalili na kuunge. Usiyejijuwa. Usiyejitambuwa.

Lakini hebu Wazanzibari natujiulize masuali mawili: kwanza, kwa nini Uzanzibari, kama mfumo wetu wa maisha, unapotea na, pili, kipi cha kukifanya ubakie na urithishwe kwa kizazi chetu?

Kuna wanaouchukulia upotevu wa Uzanzibari kama matokeo ya kawaida tu ya kuongezeka kwa mahitaji ya wakati tulionao na mwenendo wa mabadiliko yanayoukumba ulimwengu hivi sasa. Ni kanuni ya kawaida pale mahitaji yanapoongezeka, basi mabadiliko huwa lazima. Na kila panapozuka mabadiliko, kutakuwa na kupoteza baadhi ya mambo na kuingiza mengine.

Zanzibar nayo ni sehemu ya ulimwengu huu. Imepitia vipindi vingi vya mabadiliko yalichochewa na kuongezeka kwa mahitaji ya watu wake. Kwa hivyo, Uzanzibari nao, kama mfumo wa maisha, umekuwa na kubadilika na, hivyo, umeingiza na kutowa kama ilivyo desturi ya ukuwaji na mabadiliko. Zanzibar aliyoiishi Mzanzibari wa miaka 200 nyuma sio aliyoiishi wa miaka 100 baadaye na siyo anayoishi wa sasa. Na kila mmoja anapokuja, anaambiwa: “Hivi sivyo Zanzibar hasa ilivyokuwa. Hii haina tena ule Uzanzibari wetu.”

Kimsingi, sipingani na hoja hii, maana ni sawa kukuwa na kubadilika ndiyo dhati ya maisha ya kibinaadamu, na hivyo kwa mifumo yao ya maisha pia. Mwanaadamu aliyekamilika lazima akuwe na abadilike kwa kadiri mahitaji na mazingira yatakavyomsukuma huko.

Lakini suala hapa sio kukuwa na kubadilika tu, bali ni namna ya huko kukuwa na kubadilika kwenyewe, ndiko kunakoweza kupewa hadhi ya kuitwa kwa kibinaadamu. Lazima kuwe ni ndani ya mzunguko wa mwanaadamu huyo. Kumuhakikishie utukufu na vipawa vyake na kumpe utambulisho wake. Ukuwaji ni maendeleo ya kutoka pabaya kuelekea pazuri zaidi. Mabadiliko ni kupunguza yanayokirihisha na kuongeza yanayoridhisha. Kinyume chake si ukuwaji wala si mabadiliko!

Tunapopima kupotea kwa Uzanzibari wetu kwa kigezo cha ukuwaji wa mahitaji na kasi ya mabadiliko, basi hoja haiko upande wetu. Kuna muktadha mwengine zaidi ya huu wa mahitaji ya wakati na mwenendo wa mabadiliko, ambao ni kama ule anaouzungumzia Malcolm X wa kumuita Muafrika mniga, ili asikujuwe anakotoka, asiitambuwe hadhi yake na akose kujigamba kwa utukufu wake na ili, hatimaye, aweze kutumiliwa kirahisi!

Mzanzibari anapofanywa asiijuwe milki wala mamlaka yake na kaamini milki na mamlaka za wengine, anapofanywa asijitambulishe kwa asili yake na akaiga utambulisho wa wengine, huwa kwa hakika amekwisha. Anaweza kutumiliwa akatumika, anaweza kudhalilishwa akadhalilika, maana huwa amepoteza nguvu, uthubutu na mashiko ya kushika. Hana mizizi!

Nitafafanua. Zanzibar si eneo pekee ulimwenguni ambalo limekumbwa na mahitaji ya wakati na kasi ya mabadiliko. Kwa kweli kila sehemu ulimwenguni imeathirika na mifumo yake ya kijamii imelazimika kuingiza na kupoteza baadhi ya mambo, lakini hayo siyo yale ya msingi yanayozitambulisha jamii hizo. Ule utambulisho wao umebakia pale pale. Mataifa ya Asia ya Kusini ni mojawapo ya mifano hiyo.

Zanzibar, kwa bahati mbaya, ni miongoni mwa sehemu chache ambazo hoja hii ya mabadiliko na mahitaji ya wakati imetumika kama silaha ya mavamizi na maangamizi dhidi ya kila taasisi ya kijamii: kuanzia familia, utamaduni, vyombo vya habari na utawala, na matokeo yake yamekuwa ni madhara kwa jamii nzima.

Wataalamu wa Soshiolojia wanasema taasisi hizo ndizo nguzo ambazo jamii husimamia. Zinapokuwa madhubuti, basi jamii huwa imara na hudumu ikiwa kama jamii kamili. Zinapokuwa dhaifu, jamii nayo hulegea na kupoteza utambulisho wake.

Leo hii tunapolilia kupotea kwa Uzanzibari wetu, tunalia hivyo kwa kuziona nguzo hizo zilivyodhoofishwa. Tunapoiona familia imepoteza muelekeo wa Kizanzibari, utamaduni umebeba bango si lake, vyombo vya habari vinawasilisha ujumbe tafauti na kasha utawala nao hausimami imara kwa ajili ya Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari, hapo tunajihisabu kwamba tumepoteza kitu ambacho ni muhimu na kipenzi sana kwetu. Utambulisho wetu! Na kupoteza kitu hiki si jambo la kujifakharishia. Nii la kulionea haya!

Sasa tufanyeje kurudisha utambulisho wetu? Hiyo ndio mada ya wiki ijayo, inshallah!

Hii ni sehemu iliyohaririwa tena ya makala  ya Mohammed Ghassany ‘Mama Zanzibar, wanao twalilia utambulisho wetu’ iliyochapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Dira Zanzibar mwaka 2003. Makala halisi inapatikana kwenye maktaba ya mtandao wa Mzalendo.Net. 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.